Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Maana ya Kusanyiko la Kiliturujia

KUSANYIKO LA  KILITURUJIA-I
1.    Maana ya Kusanyiko la Kiliturujia:
Kusanyiko la kiliturujia ni watu walioitwa na Mungu kwa njia ya Kristo kukusanyika kama jumuiya, ili kueleza imani yao na kuikuza zaidi kupitia ushiriki wao kamili na wa dhati katika sala ya jumuiya ya Kanisa. Kusanyiko la kiliturujia linaundwa na kila mtu anayekuja kuadhimisha Misa au Sakramenti nyingine. Kusanyiko la kiliturujia kwa hakika ni dhihirisho la Kanisa katika uhalisia wake kwa wakati wa kibinadamu na wa Kimungu: ni watu waaminifu waliokusanyika kumzunguka Bwana kuadhimisha fumbo la Pasaka.
Sala za kiliturujia daima hufanywa katika umoja kwa kuwa Mwadhimishaji hunena kwa jina la wote, au huendelea na mazungumzo na watu kwamba Neno la Mungu linasomwa.
2.    Kusanyiko la Liturujia katika Mapokeo ya Kanisa:
Umuhimu wa Kusanyiko la Kiliturujia:
Kukusanyika mara kwa mara kwa ajili ya sala  ni sifa ya maisha ya Kikristo 1 Kor, 11:14; Jam, 2.1-4.
Kuna faida za Kiroho zinazopatikana katika kukukutanika, “wakutanapo wawili au watatu kwa jina langu, nipo kati yao”
Kusanyiko la kiliturujia hudhihirisha mkusanyo wa wanadamu ambao Kristo ametimiza.
Neema ipatikanayo kwenye mkusanyiko ni ya kifumbo katika kila adhimisho la Liturujia.
3.    Sifa za Kusanyiko la Kiliturujia:
i. Asili Takatifu ya Kusanyiko la Liturujia:
Kusanyiko la kiliturujia ni takatifu kwa kuwa mwanzilishi wake ni Mtakatifu, na Roho Mtakatifu analiongoza.
ii. Asili ya Agano la Kale:
Kusanyiko lilianza kwa mwito wa Abrahimu, lakini Kusanyiko rasmi linaanzia chini ya Mlima Sinai. Sheria ilitolewa, na Agano lilifanywa (Kut, 19-24, Kumb, 4.10, 9.10, 8.16, 23.1-8). Kwa Kiyunani, Kusanyiko huitwa  “Ekklesia” na kwa Kiebrania “Qahal Yahweh”. Ni Kusanyiko la Yahweh lililoitishwa na Mungu Mwenyewe (Kut, 19:17-18, Kum, 4:12-13). Yaani Mungu alikuwepo na akasema na watu wake.
iii. Kanisa la Kristo, Asli ya  Watu Wapya wa Mungu:
Kusanyiko ni Kanisa, Mt 16.18. Warithi ambao Kristo anawatuma wanaliitisha Mt, 38.18-20. Agano Jipya limetiwa muhuri kwa damu ya Kristo, Agano ambalo ni moja na la milele, na lisiloweza kubatilishwa, damu ambayo inamwagika kwa ajili ya ondoleo la dhambi. Kusanyiko hili jipya, zaidi ya lile la Agano la Kale, ni la watu wa Kifalme na Kikuhani (Kut 19.6, 1 Pet, 2.4-10, Ufu, 1.6, 5.9-10, Ufu, 20.6). Watu hao wanapaswa kutoa dhabihu ya Kiroho kwa vile wanaunda Ukuhani Mtakatifu.
iv. Kusanyiko la Kiliturujia hudhihirisha Kanisa:
Kusanyiko linadhihirisha ishara ya Kanisa, ni Kusanyiko la Kristo, yaani, Mwili mmoja wenye viungo mbalimbali. Misa katika Kusanyiko ni kumbukumbu ya dhabihu ya Kristo.
v. Mungu ndiye anayewaita watu:
Mungu ndiye mwanzilishi; wengine ni vyombo vyake tu vya utumishi. “Sio ninyi mlionichagua mimi, bali mimi niliyewachagua mimi”.  Hii inaonyesha kwamba, Mungu ndiye mwanzilishi wa kila kitu. Katika uumbaji, Mungu alianzisha kila kitu. Wanadamu walipewa mamlaka ya kutunza na kuendeleza kile ambacho Mungu tayari ameanzisha.
vi. Uwepo wa Mungu katika Kusanyiko:
“Wawili au watatu wakusanyikapo kwa jina langu, mimi nipo katikati yao, Mt, 18.20. Hii inaonyesha kwamba, Mungu anapendelea Liturujia ya kijumuiya badala ya Liturujia ya kibinafsi. Katika muktadha huu, Liturujia siyo jambo la kibinafsi.
vii.    Kusanyiko ni tarajio la Mbingu:
Kusanyiko ni taswira inayotarajia Kanisa la Mbinguni kama mtazamo katika giza la imani. Tarajio hili linaonyeshwa vyema katika kitabu cha Ufunuo. Yaani mbinguni kama Kusanyiko la Liturujia; watu ambao wamefua nguo zao katika damu ya mwana-kondoo (Ufu, 7:14)
4. Watu wa Mungu katika Kusanyiko:  
i. Kusanyiko la Watu Wote:
Kusanyiko la kiliturujia ni kwa ajili ya watu wote wanaotimiza masharti mawili. Wale ambao wameikubali imani ya Kanisa, na hawajaikana hadharani, na wale ambao wamepokea Ubatizo au angalau wanajiandaa kwa Ukatekumeni.
Wajumbe wa Kusanyiko hilo ni wakosefu wanaotafuta huruma ya Mungu. Hii ndiyo sababu sala za kawaida zinajumuisha kukiri hadharani dhambi na kuomba rehema ya Mungu. Kanisa linaanzia ngazi ya chini (familia, jumuia, Kigango, Parokia, Jimbo, Taifa, n.k.), hadi ngazi ya ulimwengu. Huo ni umoja katika utofauti.
ii. Mkusanyiko  Katikati ya Utofauti:
Moja ya sheria muhimu katika Historia ya Wokovu ni kwamba watu wapya wa Mungu lazima wawalete wanadamu pamoja, licha ya yote ambayo yanasababisha mgawanyiko (Efe 2:14, Mdo, 2:6-11). Hakuna tena aliyetahiriwa wala asiyetahiriwa, Myahudi wala mtu wa Mataifa, Myunani na Mrumi, Mtumwa na Mtu Huru. Wabatizwa wote ni wamoja katika Kristo ambaye ni Bwana wa wote. Kuna Imani moja tu, Ubatizo mmoja, Mkate mmoja tunaomega, kikombe kimoja cha damu ya Kristo na Mwili mmoja (Rum, 10:12, 1 Kor, 12:13, Gal, 3:28, Efe, 2:19, Ufu, 5:11).
Kwa hiyo, Kusanyiko ni kuleta muungano, sio mgawanyiko. Kusanyiko linaleta neema ya upendo wa kindugu na umoja.
iv. Ushiriki hai na wa Kiakili:
Waamini sio watazamaji tu, pia wanalo jukumu la kushiriki. Kushiriki Kikamilifu katika mafumbo Matakatifu na katika sala ya hadhara na kuu ya Kanisa ni chanzo cha kwanza na cha lazima cha Roho wa kweli wa Kikristo. Haki na wajibu wa Waamini kushiriki kikamilifu katika Liturujia, inatokana na asili ya Kanisa kuwa ni watu wa Kifalme na Kikuhani wanaoshiriki kadri ya hali zao, katika Ukuhani wa Kristo na kuunda mwili ambao una kazi mbalimbali, lakini hufanywa mmoja na Roho Mtakatifu.
Wanashiriki na kudhihirisha umoja huu kwa kusikiliza pamoja Neno la Mungu, wakijishikamanisha na Sala ya Mwadhimisho, kushiriki kwa njia ya mazungumzo, kuimba, matendo ya kimwili, ishara, na Misa kwa kushiriki katika Sadaka na Ushirika wa Ekaristi.
Ushiriki wa kiakili na uchaji pia unahitajika. Matendo ya kiliturujia ni ishara ambayo kwayo imani inatakiwa kugusana na Fumbo la Kimungu linalotimizwa humo; hatua hiyo inahitaji umakini wa kidini. Akili na mioyo ya Waamini lazima iendane na sauti zao wanapoimba, au kufanya mazungumzo.
Waamini lazima waifanye sala ya Mwadhimishaji kuwa yao wenyewe wanapoisikiliza. Ni lazima wasikilize Neno la Mungu kwa Uaminifu. Wakati fulani, adhimisho litawahitaji kujiweka wenyewe katika ukimya mtakatifu. Kwa hiyo, waamini lazima wapewe ufahamu wa taratibu na Maandiko hivi kwamba, ndani ya Kusanyiko hakuna mtazamaji, ila wote ni washiriki na watendaji.
v. Watu wanaoadhimisha:  
Kusanyiko linaunda adhimisho. Waamini wanakusanyika kimsingi kuadhimisha kwa shukrani tukio la Fumbo la Wokovu. Kusanyiko linaweza kufanyika kwa ajili ya uchaji binafsi kama vile litania, mikesha n.k, lakini ibada hizi za uchaji, karibu kila mara ni maandalizi ya maadhimisho ya kiliturujia.
5.    Majukumu  katika Kusanyiko:
5.1 Utangulizi:
Katika Kusanyiko, kila mshiriki huchukua sehemu hai yenye majukumu tofauti. Ni hivyo ili kudhihirisha asili ya Kanisa. Adhimisho lina Mkuu, ambaye ni Mwadhimishaji Mkuu, na kati ya Mwadhimishaji Mkuu na Waamini, kuna wasaidizi wanaofanya huduma za utumishi.
Katika adhimisho la Liturujia, kila mmoja, Mhudumu Mlei, ambaye ana ofisi ya kuhudumu, anapaswa kufanya yale tu yanayohusika na ofisi hiyo kwa asili ya ibada na kanuni ya Liturujia (VSC 28). Utofauti huu wa majukumu, hufanya Kusanyiko kuwa mwili hai ambao ni udhihirisho wa Mwili wa Fumbo wa Kristo (1 Kor, 12:12-30). Utekelezaji wa majukumu hayo tofauti unaifanya Liturujia iwe katika utaratibu madhubuti ambapo kila mshiriki anatekeleza wajibu wake ipasavyo.
5.2 Mwadhimishaji
Mwadhimishaji, ambaye ni Askofu au Padri, anaongoza Kusanyiko katika nafsi ya Kristo. Yeye ndiye anayesimamia vyema Kusanyiko, na anaongoza sala. Anafanya matendo matakatifu, anamega mkate wa Neno la Mungu na mkate wa Ekaristi kwa ajili ya watu. Nafasi yake si kwa kuteuliwa na Kusanyiko au kwa sababu ya sifa za kibinadamu, bali kwa sababu kwa kuwekwa wakfu ana sifa ya Kikuhani. Kwa nguvu ya sifa hii, anachukua nafasi ya Kristo. ‘Anatenda katika nafsi ya Kristo’. Anapoadhimisha mafumbo matakatifu, Kristo anakuwa ndani yake.
Askofu wa Mahalia ni Mwadhimishaji Mkuu kwa kuwa Utume wake ameurithi kutoka kwa Mitume. Hakuna awezaye kuongoza shughuli ya Liturujia jimboni, isipokuwa kwa amri yake na idhini yake. Kiti chake katika Kusanyiko kimewekwa hivi kwamba yeye aonekane kwamba ndiye kitovu na kiini cha Kusanyiko zima.
Mapadri , ambao ni watenda kazi pamoja na Askofu Mahalia na wanaopokea Utume wao kutoka kwake, wanaliongoza Kusanyiko mahali pake na kwa muungano naye. Hata hivyo, hawawezi kufanya maadhimisho fulani ambayo yametengwa kwa ajili ya Askofu  kwa mujibu wa taratibu za kiliturujia na sheria za Kanisa.
Shemasi, kama Padri hayupo, anaweza kuongoza na kuadhimisha ibada fulani kama vile Ubatizo, Liturujia ya Masaa, mazishi, na mengine, kulingana na Kanuni za Kiliturujia na sheria za Kanisa. Katika Kusanyiko la Dominika, ibada maalum bila Padri inaweza kutambuliwa kwa kuzingatia miongozo iliyotolewa.
Itaendelea makala ijayo.

Rate this item
(0 votes)

Leave a comment

Make sure you enter all the required information, indicated by an asterisk (*). HTML code is not allowed.