Dar es Salaam
Na Salum Mgweno-SJMC
Soko la Kilamba katika Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam, limegeuka gofu baada ya kutelekezwa na wafanyabiashara kwa takriban miaka miwili.
Moja ya sababu za kulikacha soko hilo ni ubovu wa barabara, hali inayowalazimu wananchi wa maeneo hayo kutembea umbali mrefu kufuata mahitaji yao katika masoko ya mbali.
Akizungumza na Tumaini Letu, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kilamba Nzasa B, Hassan Ugando alisema kuwa soko hilo lenye vizimba takribani, 72, lilianzishwa tangu mwaka 2005 kwa gharama ya Shilingi milioni 100, ambapo Shilingi milioni 80 ni kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, huku Shilingi milioni 20 zikiwa ni nguvu za wananchi, limekuwa likitumika msimu kwa msimu na kisha kutelekezwa, ambapo kwa mara ya mwisho kutumiwa na wafanyabiashara ilikuwa mwaka 2021.
“Mwaka 2020 kwenda 2021, bado kulikuwa na wafanyabiashara kadhaa ambao pia waliondoka. Kwa hiyo kama unavyoona, wamebaki wale wachache wenye vibanda pembeni mwa soko na yule wa buchani tu,” alisema Ugando.
Ugando alisema kuwa miongoni mwa sababu za soko hilo kukosa ustawi wa kibiashara baada ya kukamilika ujenzi wake, ni kwamba waliokabidhiwa vizimba vya biashara hawakuwa wafanyabiashara.
Kwa mujibu wa Ugando, pia ugawaji wa vizimba hivyo, ulitoa kipaumbele kwa wananchi walioshiriki bega kwa bega ujenzi wa soko hilo. Hivyo licha ya wengi wao kuwa siyo wafanyabiashara, walichukua kwa lengo la kukodisha ili wapate pesa.
Ugando alisema kuwa ubovu wa barabara pia umechangia watu kulikimbia soko hilo, na hivyo kuendeelea kusalia kuwa gofu na mapango ya ndege.
Ugando amelieleza Tumaini Letu kuwa kitendo cha wafanyabiashara kukimbilia maeneo ya barabarani wakiamini kuwa ndiyo sehemu yenye mzunguko mzuri wa biashara kutokana na idadi kubwa ya watu, imedhoosha soko hilo.
Naye Emmanuel Pascal, mfanyabiashara wa nyama pembezoni mwa soko hilo, aliiomba Serikali kukarabati vyoo na huduma ya maji, ili kuweka sawa mazingira ya soko hilo.