DAR ES SALAAM
Na Mathayo Kijazi
Imeelezwa kuwa Mungu ameumba uoto wa asili, maji, na viumbe malimbalimbali duniani ili visiharibiwe, kwani chanzo cha kutoka kwa mabadiliko ya tabianchi ni kuharibiwa kwa mazingira.
Hayo yalisemwa hivi karibuni na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddeus Ruwa’ichi wakati akihubiri katika Adhimisho la Misa Takatifu ya kutoa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara kwa vijana 42 wa Parokia ya Mtakatifu Yohane Mbatizaji – Msongola ‘B’, jimboni humo.
“Mnaposikiliza taariba ya habari, au mnaposoma kwenye magazeti, na kwenye vilongalonga vyenu, mnaona mahali pengi kuna habari juu ya Tabianchi. Hayo mabadiliko ya tabianchi yanamuumiza mwanadamu, yanaviumiza viumbe, yanatusambaratisha,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi:
“Sasa hayo mabadiliko ya tabianchi hayakutokea hivi hivi, kuna mkono wa mtu. Sasa msiseme kwamba Askofu anashabikia uchawi, ninaposema kuna mkono wa mtu, sina maana kwamba kuna mchawi, kama kuna mchawi ni sisi, yaani mimi na wewe. Mkono unaovuruga nchi na kufanya kuwe na mabadiliko holela, ni mkono wa mwanadamu mvurugaji, mwanadamu mchafuaji.”
Askofu Ruwa’ichi aliwasisitiza kuwa Wakristo wanatakiwa kutodhoofisha uoto wa asili ulioumbwa na Mungu, akisema, “Mnatambua kwamba pale mlipofyeka mkaondoa uoto wa asili, pamedhoofika. Kwa hiyo Mungu aliyeumba uoto wa asili, aliyeumba miti, aliyeumba maji, aliyeumba majani, aliyeumba wanyama na ndege, ametaka vitu hivi vitumiwe kwa utaratibu kusudi vimhifadhi mwanadamu kwa vizazi vyote.”
Aliongeza kuwa sehemu yoyote yenye joto kali lililopitiliza, hakuna mwanadamu anayeweza kuishi wala kustahimili hapo, hivyo yeyote anayevuruga na kuharibu mpangilio huo wa asili, anajitakia maangamizi.
Wakati huo huo Askofu Mkuu Ruwa’ichi aliwasisitiza Waamini kujenga urafiki na maumbile, akiwataka kuyaratibu, kuyatumia kwa uangalifu na staha kama Mwenyezi Mungu alivyoagiza.
Kwa mujibu wa Askofu Mkuu, Waamini wanapaswa kuwa na mahusiano mazuri kati yao na Mungu, akiwasihi wapende kujenga mahusiano safi, hai, na yenye tija na Mungu wao, kwani wakitenda hivyo, watakuwa wanajitahidi kuzingatia anayotaka Mungu.
Wakati huo huo, Askofu Mkuu huyo aliwaasa waamini daima kuwa watu wa amani, wakiwa viumbe wenye kupendana na kusaidiana, badala ya kusakamana.
Awapa darasa Waimarishwa
Akizungumzia kuhusu Waimarishwa hao, Askofu Mkuu Ruwa’ichi aliwataka vijana hao kufahamu kwamba wanapompokea Roho Mtakatifu, wanakamilishwa, na hivyo wanatumwa kuifanya kazi ya kuitangaza Habari Njema kwa watu wote.
Paroko na Paroko Msaidizi, kwa kushirikiana na wazazi parokiani hapo, waliagizwa na Askofu Mkuu Ruwa’ichi kuendelea kuwapatia mafunzo ya kiimani vijana hao ili wakue katika misingi yenye maadili mema.