DAR ES SALAAM
Na Eva Paul – TUDARCO
Wananchi wa Mtaa wa Mikongeni, Manisipaa ya Ilala Jijini Dar es Salaam, wameiomba Serikali kuimarisha ulinzi na usalama ili kudhibiti vitendo vya uhalifu vilivyokithiri katika eneo hilo.
Akizungumza na gazeti la Tumaini Letu katika mahojiano maalumu, Mjumbe wa nyumba kumi katika mtaa huo, Sara Malimbwi, alisema kuwa mtaa huo unakabiliwa na makundi ya vijana wanaovamia watu majumbani, na kuwaibia mali zao.
“Ni watoto wadogo tu, ambao walipaswa wawe shule, lakini wamejiingiza kwenye makundi ya wahuni, yaani ukiwaona utasikitika, kwani ni watoto wadogo, wengine hata darasa la saba hawajamaliza, lakini tayari wameshaacha shule, kutwa wanashinda vijiweni… Sisi kama wazazi tunaumia sana kuona watoto wanaharibika kiasi hiki, lakini hatuna cha kufanya,” alisema Sara.
Aliwasihi wazazi na walezi kuwaonya na kuwadhibiti watoto wao ili waache vitendo vya wizi.
Baadhi ya wananchi hao walisema kwamba vijana hao wanaotembea kwa makundi, wamekuwa wakiwavamia wananchi, hata nyakati za mchana.
Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa eneo hilo, walisema kuwa wanashangazwa kwa kukithiri uhalifu huo, licha ya kuwepo kwa ulinzi shirikishi unaochangiwa na malipo ya Shilingi 1000/= kwa mwezi kwa kila kaya.
“Tunalipa pesa ya ulinzi, lakini bado tunaibiwa, sasa walinzi wanafanya kazi gani?...” alihoji Hassan Selemani mkazi wa mtaa huo.
Naye Anna Lucas, mkazi wa eneo hilo alisema kuwa vitendo hivyo vimewachosha, kwani vimekithiri mtaani hapo.