DAR ES SALAAM
Na Mwandishi wetu
Wakristo wametakiwa kuepuka kuwapenda wanzao kwa sababu ya vitu au misaada wanayopata, bali wafanye hivyo kwa sura na mfano wa Mungu.
Hayo yalisemwa hivi karibuni na Padri Dickson Sambala- OCARM, wakati akihubiri katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Kuwashukuru Wanaparokia ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli – Bunju, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, kwa kumlea katika kipindi cha Uchungaji wake, iliyoadhimishwa parokiani hapo.
“Unaposali, unatengeneza matunda ya upendo, kwani unapopenda, unatengeneza matunda ya huruma kwa ajili ya kuwahudumia wengine, na unapowahudumia wengine, unatengeneza amani ndani ya mioyo ya watu….;
“Unatakiwa kuondoa matabaka kati ya walio nacho na wasio nacho. Unawaheshimu watu kwa sababu wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, lakini siyo kwa sababu ni matajiri, siyo kwa sababu wanatusaidia hiki au kile,” alisema Padri Sambala.
Katika homilia yake, Padri Sambala aliwaasa Wakristo kuepuka kuwa na upendo wa masharti, kwani upendo huo huchagua baadhi ya watu.
Aliongeza kuwa upendo wa kweli ni ule wa kidugu unaowafanya watu kuwa kitu kimoja, na kuwafanya kupokea baraka za Mungu.
Aidha, Padri Sambala aliwashukuru waamini wa Parokia hiyo kwa ushirikiano waliompatia na kuipongeza Tumaini Media kwa kazi kubwa ya uinjilishaji kupitia vyombo vyake vya habari.
Naye Roselinda Msele, Katibu wa Kamati ya Liturjia Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli – Bunju, aliwaomba watu wenye mapenzi mema kuchangia ujenzi wa kanisa jipya la Parokia hiyo, ili ukamilike kwa wakati uliopangwa.
Naye Diana Peter, Mlezi wa Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu wa Parokia hiyo, aliwasihi wazazi kuendelea kuwalea watoto katika maadili ili kupata watu wema.