DAR ES SALAAM
Na Mathayo Kijazi
Paroko wa Parokia ya Bikira Maria Mama wa Rozari – Bombambili, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Sheejan Kallarakkal- MSFS, amesema kwamba uwepo wa wazee katika Kanisa, jamii, na hata familia, ni hazina kwa sababu wana uzoefu wa kimaisha.
Padri Sheejan alisema hayo wakati akihubiri katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Shukrani kwa Mungu kwa Wazee na Wastaafu wa Dekania ya Pugu, kwa mengi aliyowatendea, iliyoadhimishwa parokiani hapo.
“Uwepo wao wazee katika Kanisa, jamii, na hata familia, unaleta maana kubwa, na una faida kwa sababu wana uzoefu mkubwa katika kusimamia mambo…Kwa hiyo, ukiwa mzee una fursa fulani katika maisha yako, hivyo tumia uzee wako kurithisha imani kwa vijana na watoto,” alisema Padri Sheejan.
Aidha, aliwakumbusha wazee kutambua kwamba wana jukumu la kusambaza ukweli na mafundisho ya Kanisa kwa vijana, kwani wanakubalika kwa matendo na sauti zao.
Awali akitoa homilia yake, Padri Sheejan aliwaomba wazee hao kuwakemea vijana wanapokengeuka, ili kujenga heshima kwa watu wote.
Aliwasihi wazee na wastaafu hao kumwomba Mungu ili waendelee kuwa watu wa hekima na maarifa, yaani busara ndani ya Kanisa na jamii zao kwa ujumla.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Wazee na Wastaafu wa Dekania ya Pugu, Cosmas Sokoni, aliwashukuru wazee wote walioshiriki Misa hiyo, akiwasihi wazidi kushirikiana ili chama cha Wazee na Wastaafu katika Dekania hiyo kikue zaidi.
“Kwanza, nichukue nafasi hii kuwashukuru wazee wenzangu wote tulioshiriki katika Misa hii Takatifu. Niwaombe tu kwamba tuzidi kushirikiana ili chama cha Wazee na Wastaafu katika Dekania yetu ya Pugu, kizidi kukua na kusonga mbele,” alisema Sokoni.
Aidha, Sokoni aliwahimiza viongozi wenzake kushirikiana na kusaidiana, ili wawe na umoja uliokamilika, na hivyo waweze kwenda pamoja.