Mtwara
Na Mwandishi wetu
Paroko wa Parokia ya Yesu Kristo Mkombozi - Magomeni, Jimbo Katoliki la Mtwara, Padri Silvanus Chikuyu, amesema kuwa mtu yeyote anapouona Msalaba, anatakiwa asipite bila kutafakari upendo wa Yesu Kristo kwa wanadamu.
Padri Chikuyu alisema hayo wakati akitoa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Sikukuu ya Somo wa Kutukuka kwa Msalaba, Kigango cha Lyenje, Parokia ya Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni – Luagala, Jimbo Katoliki la Mtwara.
“Na naomba kila mmoja anapouona Msalaba, asiishie tu kuuona na kupita zate, bali atafakari. Katika msalaba tuone mambo mawili makuu, kwanza kabisa tuone upendo wa Mungu kwetu sisi wanadamu….hakuna upendo ulio mkuu kama wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya wengine.
“Yesu Kristo ametupenda, akatoa uhai wake kwa ajili yetu sisi, ili sisi tuwe nao tele. Hilo ni jambo kubwa sana, usiupite tu Msalaba hivi hivi bila kutafakari upendo wa Mungu kwa wanadamu wote. Jambo la pili ni utii na unyenyekevu wa Yesu Kristo, ambaye alikubali kuachilia hali yake ya Kimungu, akajinyenyekesha akatwaa hali yetu ya kibinadamu,” alisema Padri Chikuyu ambaye pia alikuwa mgeni rasmi.
Aidha, Padri Chikuyu aliongeza kuwa ni haki kwa kila Mkristo kuwa na msalaba nyumbani kwake, kwani kwa kufanya hivyo, milango ya baraka na mafanikio itapatikana katika maisha yao.
Padri huyo alisema kuwa wapo baadhi ya Wakristo ambao wanaishi na wenza wao katika familia, lakini wamekuwa wagumu kufunga ndoa, akisema kuwa ni vyema wakawa na misalaba majumbani mwao, ili baraka ziwafikie, na waweze kufunga ndoa.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia ya Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni – Luagala, jimboni humo, Padri Andrew Chitanda alisema kuwa amefurahi kuona maadhimisho hayo yamekwenda vizuri.
“Maadhimisho haya yatie hamasa kwa ndugu wengine wote kutoka Parokia zote, Wakristo kutoka Vigango mbalimbali, kutoka Jumuiya mbaimbali, ili waweze kuthamini na kuadhimisha siku maalumu za Somo wa Kigango, au wa Parokia. Kwa hiyo, nawahisi Vigango vingine waweze kuiga mfano huu,” alisema Padri Chitanda.
Kwa Upande wake, Sista Elvira Lilungulu wa Shirika la Masista wa Mkombozi, Jimbo Katoliki la Mtwara, aliwaomba wazazi kuwaruhusu watoto wao wa kike na wa kiume wajiunge katika Mashirika mbalimbali ya Kitawa ili wamtumikie Mungu, kwani Mungu ndiye anayewaita kwa ajili ya kumjua na kumtumikia.
Naye Mwenyekiti wa Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) wa Kigango cha Kutukuka kwa Msalaba - Lyenje, Regina Mtanda, aliwaasa akinamama kuwalea watoto katika maadili mema ili wale wenye wito waweze kuikimbilia miito hiyo.