VISIGA, PWANI
Na Mwandishi wetu
Wabatizwa nchini wametakiwa kuitambua hadhi yao, kwani wao ni hekalu la Mungu, hivyo hawatakiwi kuligeuza hekalu hilo kuwa jalala la dhambi.
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi alitoa wito huo wakati wa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Kutabaruku Kanisa la Seminari Ndogo ya Mtakatifu Maria – Visiga, mkoani Pwani.
“Tusimshangae sana Suleimani, tuchote fundisho kutoka kwake, kwa nini? Kwa sababu hata sisi tuna kibali machoni pa Bwana, siyo tu kwamba Mungu ameturuhusu tujenge hekalu, bali ametupa haki ya kuwa hekalu lake. Kila Mbatizwa anayo hadhi ya kuwa hekalu la Roho Mtakatifu…
“Kwa hiyo, ewe Mbatizwa, tambua hadhi yako, tambua wito wako, tambua heshima yako, na tunza utakatifu wako mbele za Mungu. Usikubali kukengeuka na ukaligeuza hekalu la Mungu kuwa jalala la dhambi,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
Aidha, Askofu Mkuu aliwaasa Waamini kumbeba Kristo na kumpeleka kwa wengine, kwani kwa kufanya hivyo, watakuwa wameinjilisha na wamekuwa wajumbe wa Habari Njema katika maisha yao.
“Maria huyu ni mfano wetu, kwani sisi pia tunaitwa tumbebe Kristo na tumpeleke kwa wenzetu. Kwa maneno mengine, tunaitwa tuwe wainjilishaji, tuwe wajumbe wa Habari Njema,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
Aliwashukuru Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA), kwa majitoleo yao yaliyoweza kujenga kanisa hilo lililotabarukiwa, akisema kuwa kujituma kwao na kwa ukarimu wao, ndiko kumefanikisha kukamilika kwa ujenzi huo.
Vile vile, Askofu Mkuu aliagiza kuwa kanisa hilo lililotabarukiwa, lisigeuzwe kuwa ukumbi, bali liwe tu kwa ajili ya mambo ya Mungu na Taifa lake Takatifu.
Wakati huo huo pia, Askofu Mkuu Ruwa’ichi aliialika Jumuiya ya Seminari kulitunza kanisa na altare hiyo, ili viendelee kutumika kama ilivyokusudiwa.
Aliwataka Waseminari kutokuona aibu ya kutoa ushuhuda wao, bali wajivunie kwamba wamepata heshima ya kuwa Wakristo, hivyo hawana budi kuutunza uwakfu wao.
“Kwenu Waseminari, tunza uwakfu wako, jilinde kama hekalu Takatifu, toa harufu ya utakatifu na usione aibu kutoa ushuhuda wa Ukristo wako. Jivunie ya kwamba umepata heshima ya kuwa Mkristo, ishi heshima hiyo na shuhudia heshima hiyo na lijenge Kanisa la Kristo,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
Kwa upande wake, Gombera wa Seminari Ndogo ya Visiga, Padri Philip Tairo, alisema kuwa wanamshukuru Mungu kwa kuwapa nguvu ya kufanya kazi hiyo ya ujenzi wa kanisa ambayo waliianza Novemba mwaka 2022.
Naye Mwenyekiti WAWATA jimboni humo, Stella Rwegasira alimshukuru Askofu Mkuu kwa kuunganisha tukio lao la shukrani pamoja na la kutabaruku kanisa hilo, huku akisema kuwa kwao kama WAWATA, hiyo ni siku ya furaha kubwa.