Na Joseph Mihangwa
LIPOISHIAI
...Ni utawala wa Chama dola na Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Ingawa tumeingia mfumo wa Vyama vingi, Katiba inanuka harufu ya Chama kimoja kiasi cha watu wengine kukiita Chama kilichoshinda “Chama dola”, wakati ukweli dola si ya Chama, bali ni ya wananchi!.
ENDELEA...
Mhimili wa Chama na Ujamaa kati ya mitatu umekwishavunjika; Sera za Ujamaa na kujitegemea zimevunjwa na Azimio la Zanzibar mwaka 1992; nao mfumo wa Chama kimoja umeuawa na mfumo wa Vyama vingi vya siasa tangu mwaka 1992. Mfumo huu na ule wa uchumi huria, havikuwa katika mawazo ya watunga Katiba ya 1977. Ndiyo maana, Katiba ya sasa inakinzana kwa sehemu kubwa na mengi yanayotokea nchini.
Tunachosema hapa ni kwamba madaraka makubwa ya Rais asiyeambilika, yalidumu na kuweza kufanya kazi tu kwa msaada wa mafiga mawili yaliyovunjika – [Ujamaa na Chama kimoja], na kwamba, maadam sasa msaada huo haupo tena, madaraka makubwa ya Rais yataendelea kuelea na kupwaya kwa vigezo vyovyote vya utawala wa Sheria, demokrasia na utawala bora. Na pale Rais atajaribu kutenda kwa ubunifu wake binafsi kinyume na haya, hataepuka kuitwa “dikteta”.
Tunaambiwa, nchi yetu inafuata mfumo wa Utawala wa “Westminster”, unaozingatia Mgawanyo wa Madaraka. Chini ya mfumo huo, muhimili mmoja wa Serikali unakatazwa kuingilia kazi za muhimili mwingine ili kila muhimili uchunge mwenendo wa muhimili mwingine. Dhana hii sasa ipo kwa jina tu kama tutakavyoona hivi punde.
Marekebisho ya hapa na pale yaliyofanyika baadaye kwenye Katiba hayakugusa madaraka ya Rais, lakini badala yake, kadri sekta ya umma ilivyozidi kupanuka na ukuu wa mfumo wa Chama kimoja kujiimarisha, ndivyo jinsi madaraka ya Rais yalivyozidi kuwa makubwa.
Aliweza kutumia nyundo ya Chama wakati huo huo kama Rais wa Nchi, na aliweza kutumia pia ngao ya Rais kulinda Chama wakati huo huo kama Mwenyekiti wa Chama. Rais wa Nchi na Mwenyekiti wa Chama Taifa kilikuwa na hadi leo ni kitu kimoja. Na ndiyo sababu ya Chama madarakani kuitwa “chama dola”! Kwa sababu hii, madaraka ya Rais yalipanuka kinyemela kuanzia na Katiba ya Nchi, hadi kwenye Katiba ya Chama cha Siasa tawala. Kwa sababu hii, Rais asiyeambilika [The Imperial Presidency], anachukuliwa kama moja ya nguzo au misingi mikuu mitatu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, inayoendelea kutumika hadi leo.
Uhalali wa madaraka makubwa ya Rais kwa mtazamo wa Watawala wa enzi hizo, ulikuwa ni kuharakisha maendeleo kwa njia ya “udikteta” wa Mkuu wa Nchi, ili asiulizwe ulizwe. Mtazamo huu unadumu hadi leo.
Na katika kutekeleza hilo, Katiba ilitungwa kwa lengo la kuweka madarakani mtawala mwenye nguvu za imla, kwanza kuonesha kwamba Watanganyika sasa walikuwa huru kuweza kuendesha mambo yao wenyewe.
Pili, ilikuwa ni kuwezesha Serikali kuingilia kikamilifu [na bila ya kuhojiwa] katika maisha ya kijamii na kiuchumi ya wananchi, ili kuharakisha maendeleo kwa nguvu na imla ya kiutawala kwa “kushikisha adabu” waliohoji mwenendo wa nchi na wa watawala katika “kusukuma gurudumu la maendeleo.”
Maandalizi ya uchaguzi wa kwanza wa Rais asiyeambilika yalianza Juni 18 mwaka 1962 kwa kuandikisha wapiga kura 1,800,000 katika majimbo 50 ya uchaguzi. Wagombea walikuwa wawili – Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wa Chama cha TANU, na Bwana Zuberi Mtemvu, Rais wa Chama cha African National Congress – ANC. Uchaguzi ulifanyika Novemba 1, 1962 ambapo Mtemvu alishindwa vibaya kwa kupata kura 21,276, na Mwalimu Nyerere alipata kura 1,127,978.
Kuanzia hapo, Katiba ya nchi imekuwa ikiandikwa au kurekebishwa kukiwa na uwepo wa Rais, Mwalimu Nyerere vichwani mwa Waandishi wa Katiba. Hali haijabadilika. Katiba yetu [ibara ya 63] inamfanya Rais kuwa sehemu ya Bunge la nchi kama njia ya kudhibiti demokrasia, kinyume na dhana ya Mgawanyo wa madaraka. Na ingawa mamlaka yote ya kutunga Sheria yamo mikononi mwa Bunge [ibara 64], lakini muswada wa Sheria hauwezi kuwa Sheria mpaka utiwe sahihi na Rais. Hakuna muda maalum aliopewa Rais kwa ajili hiyo; anaweza kukalia muswada kwa muda wowote atakavyo, kana kwamba yuko juu ya Wananchi kupitia Bunge.
Endapo atakataa kutia sahihi muswada asioutaka, na Bunge likashikilia msimamo wake juu ya muswada huo, Rais ana uwezo wa kulivunja Bunge na kuitisha uchaguzi mpya. Haya ni madaraka makubwa mno kwa Rais dhidi ya wawakilishi wa wananchi. Maana yake ni kwamba ingawa Bunge laweza kupitisha Muswada wa Sheria, ukweli Rais ndiye anayetunga Sheria kwa sababu ana hiari ya kukataa au kukubali Muswada wa Bunge na asiulizwe.
Rais anapogeuka kuwa Mtunga Sheria, Bunge lifanye kazi gani? Ili kulinda hadhi na ukuu wa Bunge linalowasilisha wananchi, busara inaelekeza Bunge lidhibiti bajeti yake, Tume yake ya Utumishi ina uwezo wa kupitisha miswada kuwa Sheria inapotiwa sahihi na Spika.
Kama ilivyokuwa kwenye Katiba ya Jamhuri [1962] kwa Rais kuongoza nchi atakavyo, na kuwa halazimiki kupokea ushauri wa mtu yeyote, Katiba ya sasa [ibara 37] bado inampa ridhaa hiyo, na hawezi kuhojiwa au kushtakiwa kwa vitendo vyovyote alivyofanya akiwa Rais na baada ya hapo [Ibara 46]. Pengine ni kwa sababu hii zama zetu, kumekuwa na vitendo visivyoendana na maadili ya taifa kwenye Ikulu bila ya woga, vilivyomfanya Baba wa Taifa apige kelele kwa kusema “Ikulu ni mahali patakatifu, panatakiwa paheshimiwe”, na akaonya pasigeuzwe pango la wafanyabiashara na walanguzi.
Kama lengo la kuwepo mihimili mitatu [Utawala, Mahakama na Bunge], ni pamoja na kuimarisha demokrasia, demokrasia itatoka wapi mhimili wa utawala unapodhibiti mihimili mingine?. Inapokuwa hivyo, kwa nini tuendelee kudai tunafuata mfumo wa demokrasia wa kibunge [Parliamentary Democracy], wakati vitendo vinaonesha kinyume chake?
Rais ndiye anayeteua Jaji Mkuu na Majaji [wanaosimamia mhimili wa Mahakama], Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Viongozi wengine. Kitendo cha kuteua chenyewe pekee kinamaanisha kwamba wateule hao wanawajibika kwake. Na kwa sababu hiyo mhimili wa kulinda haki [Mahakama], unawajibika kwa Rais pia. Hii inakwenda kinyume na dhana nzima ya mgawanyo wa madaraka na ya utawala wa Sheria kwa ujumla, kwa Rais kudhibiti Bunge na Mahakama, pamoja na Watendaji wake.
Kwa kusema haya, hatumaanishi kwamba kwa watawala kuvuka mipaka ya Kikatiba mara kwa mara hakuzai matunda siku zote, bali kwamba panatakiwa tamko thabiti lenye kueleweka juu ya aina ya demokrasia tunayopaswa kufuata kuweza kujipima na kuweza kupimwa pia kimataifa. Uhuru na demokrasia si lelemama, bali “UHURU”, kama alivyosema Baba wa Taifa, “ni KAZI”.
Tafsiri ya neno “demokrasia” ni pana kwa kuzingatia mahali na mazingira ya nchi. Lakini, kama Katiba ya Nchi ni hati yenye “utakaso”, na pia dira na ramani ya madaraka ya kuzingatiwa na kila mtu, basi, mfumo unaosimikwa na Katiba hiyo unapaswa kufahamika, kuzingatiwa na kuheshimiwa na wote; kinyume chake Katiba na demokrasia inageuka kuwa kejeli kwa wananchi wanaoitunga wakitarajia kwa matarajio kuona inafanya kazi. Ilivyo sasa, nchi yetu inafuata mfumo gani wa demokrasia: demokrasia ya [ukuu wa] kibunge, demokrasia ya kinasaba au ukuu wa kivikundi kwa misingi ya vyama vya siasa?
Tuseme nini zama hizi za siasa na uchumi huria na kwa Serikali kuachia nguvu za “soko” kusimamia sera na uchumi wa nchi na hivyo maisha ya watu, inapotokea mhimili wa Bunge na Utawala kuungana kuwa kitu kimoja?. Uhuru wa Mahakama utatoka wapi, kwa mfano, kwa kulazimisha chungu cha mstakabali wa nchi na demokrasia kukaa juu ya mafiga mawili badala ya matatu?
This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.
0713-526972