Katika safu hii wiki kadhaa ziliyopita, tulisoma Historia ya Kanisa la Misri na Uinjilishaji wa Misri na Kanisa la Kaskazini mwa Afrika pamoja na kuangazia Uislam ulivyoingia Afrika. Leo tusome jinsi Uislam ulivyoiteka Afrika Kaskazini. Sasa Endelea…
Baada ya dola ya Kirumi Magharibi kuanguka, Wavandali waliokuwa wameiteka Afrika ya Kaskazini, walishindwa na Kaizari wa Mashariki katika dola ya Kostantinopoli. Kaizari alimweka gavana kutawala kwa niaba yake.
Mwaka 647 Gavana Gregori wa Kartago aliwaasi wakubwa zake wa Konstantinopoli. Waislamu walipokuja toka Misri chini ya Ukba Ibn Nafi, alidhania wanakuja kumsaidia dhidi ya Konstantinopoli, hivyo akawaunga mkono wakaingia kwa urahisi.
Baadaye walimgeuka na kuteka Afrika ya Kaskazini. Wakristo Wazungu yaani wenye asili ya Ulaya walikimbilia Ulaya na wakabaki Waberba wenye asili ya Afrika, kutetea Ukristo na nchi yao.
Mwaka 711, Mussa alimtuma Tarik (riq ibn Ziyd) jemadari wa Kiberba aliyeongokea Uislamu na jeshi lao la watu 7,000 kushambulia Uhispania. Walipoanza kupata mafanikio naye alikwenda na jeshi lake, wakateka pamoja Uhispania.
Katika kugawanya nyara hizo, Waarabu na Waberba wakawa marafiki. Guba la Gilbraltar ni ukumbusho wake ‘Gebel al Tarik’. Waberba wengi waliongoka na kuwa Waislamu kwa sababu bila kuwa Mwislamu, wasingepata sehemu ya hizo nyara na marupuuupu mbalimbali.
Mwishoni mwa karne ya 8, Afrika ya Kaskazini yote ilishakuwa ya Kiislamu. Wakati wa Mtakatifu Augustino, Afrika ya Kaskazini palikuwepo na maaskofu 700, lakini walipovamia Waislamu walibakia 35, na katika karne ya 12 walikosa maaskofu watatu wa kumweka wakfu mwenzao; na karne ya 14 hapakuwepo hata askofu mmoja.
Tofauti na Misri, ambapo ingawa lilidhoofishwa, bado Wakristo wapo licha ya unyanyasaji. Kanisa huko Afrika ya Kaskazini, maarufu kwa watakatifu na wanateologia kama Sipriani, Tertuliani na Augustino, lilitoweka kabisa.
Kosa kubwa la kwanza la Kanisa hilo ni kwamba lilijipenda na kujiendeleza kwa ndani, lakini likasahau kuinjilisha. Dini ilibaki tu katika mwambao wa dola ya Kirumi, tofauti na Misri waliotoka nje na kwenda Nubia hadi Uhabeshi.
Vilevile, dini ilibakia katika utamaduni wa kikoloni wa Kilatini hata wakawa Walatini kuzidi Roma. Hata mtakatifu Augustino ambaye mama yake alikuwa Mberba, hakuandika chochote katika lugha yao au kuingiza utamaduni wake katika Ukristo.
Wazawa walijua Ukristo kama waliingia utamaduni wa wakoloni wao. Hivyo wakoloni walipoondoka na lugha ya Kilatini, Dini ikatoweka pamoja nao. Misri waliendeleza lugha yao na kutengeneza ibada ya Kikopti, tofauti na Kigiriki.
Kanisa lisiloinjilisha na kutamadunisha, hufa. Hivyo, ile tabaka ya juu ya Walatini ambao ndio walikuwa Wakristo walipovamiwa na Waislamu, wao walikimbilia Ulaya pamoja na Maaskofu na Mapadre. Hili ni somo kubwa kwetu, Kanisa ili lidumu lazima liingie katika utamaduni na masiha ya kila siku ya watu, la sivyo litabaki kama vazi la Jumapili.
Waislamu katika Nubia (Sudan ya Sasa):
Baada ya kuiteka Misri, mwaka 641, Abdallah Ibn Saad aliishambulia Nubia. Ili kuhimili mashambulio hayo, falme mbili za Kaskazini Nobatia na Makuria ziliungana na kuwa ufalme wa makuria.
Kwa pamoja, zilishinda dhidi ya mashambulizi. Baadaye ufalme wa Makuria ulifanya umoja na ule wa Kusini wa Alodia na kupata nguvu kiasi kwamba mwaka 737 walituma kikosi hadi Aleksandria, Misri kumtoa mahabusu Patriarka aliyekuwa ametekwa na Waislamu.
Miaka kati ya 700 hadi 1250, kilikuwa kipindi cha maendeleo mazuri kwa Nubia. Walijenga makanisa mazuri, na hata mengine yamevumbuliwa na wachimbaji wa mambo ya kale. Alodia peke yake ilikuwa na makanisa zaidi ya 400 na monasteri nyingi. Pamevumbulika na maandishi mengi waliyoyaacha yakielezea ibada zao, na hasa sala.
Mwaka 1172 Misri ilitawaliwa na Waturuki wa Mamluki ambao walikuwa na nguvu na vilevile wakatili sana. Hawa walizonga Nubia, na ili kujihami, Misri iliweka Waislamu Kaskazini mwa Makuria kama ugo dhidi ya mashambulizi.
Bahati mbaya Nubia ilikuwa imekatwa kutoka ulimwengu mwingine wa Wakristo, na baadaye pakawepo mfarakano katika urithi wa wafalme. Hata hivyo waliweza kuwahimili Waislamu hadi mwaka 1504 ufalme ulipotekwa na Waislamu kutoka Misri.
Kwa miaka 1,000 walikuwa na Ukristo imara. Wamisionari waliporudi mwaka 1845 hawakukuta alama zo zote za Ukristo. Ilibidi waanze upya kati ya Waafrika weusi wa Sudan ya Kusini.
Uhabeshi (Ethipia ya sasa) na Uislamu
Uhabeshi ilikuwa na bahati ya kunusurika kutekwa na Waislamu. Sababu za kunusurika kwake kwanza ni kwamba Muhammad alipofukuzwa kutoka Mekka, Waislamu wengine walikimbilia Axum, Mji Mkuu wa Uhabeshi na kupokelewa vizuri.
Kwa sababu hiyo, Muhammad aliagiza katika Korani kwamba Uhabeshi isishambuliwe, labda kama ni kujikinga. Mwanzoni agizo hilo liliheshimiwa sana. Pili, nchi ya Uhabeshi iko milimani na si rahisi kuifikia na kuishambulia.
Wote waliozunguka Uhabeshi walitekwa na Waislamu, na yenyewe ikabaki kama kisiwa. Hata hivyo, Waislamu wengine waliingia mipakani na kuishi pembezoni na Waislamu wafanya biashara walioingia ndani walipeleka pamoja nao mawazo ya dini yao.
Mara nyingine ilikuwa vigumu kumpata askofu (Abuna) kutoka Misri, na hivyo kukaa miaka bila askofu au uongozi imara. Ili kujikinga na Waislamu, Wakristo walikimbilia zaidi ndani na milimani.
Kwa kwenda ndani ilisaidia kuinjilisha wazawa wa ndani ya nchi, na kuingiza zaidi utamaduni wao katika maisha ya dini. Ndani ya nchi yalikuwemo makabila ya Wahabeshi (Abyssinia), na mchanganyiko ukazaa utamaduni mpya wa Kihabeshi wenye lugha ya Amharic, ambayo sasa ndiyo lugha rasmi ya taifa, lakini lugha ya ibada iliendelea kuwa ‘Gaez’, lugha ya zamani ya Axum.
Mwaka 1270 Mfalme Yekuno Amlak (1270 - 85) na baadaye Mfalme Amda Seyon (1312 - 1342), walifufua kwa nguvu ukoo wa ufalme wa Suleman ambao ulikuwa umepoteza madaraka kwa Wazagwe tangu mwaka 1137.
Mfalme Zara Yokob (1411-1468), alifikisha katika kilele ustawi wa ufalme wa Uhabeshi. Akitaka kuimarisha nguvu zake dhidi ya Waislamu Wasomalia waliosaidiwa na Waturuki, alituma ujumbe Roma kwa Papa kuomba msaada.
Kama Konstantino kwa Warumi, naye alilazimisha ustaarabu wa Kikristo kwa Wahabeshi wote hata kwa wapagani, yakiwemo maadili ya Kikristo kama ndoa ya mke mmoja. Mkuu wa Kanisa la Uhabeshi alikuwa ni ‘Abuna’ aliyetumwa kutoka Misri kama kiungo cha umoja na Kanisa mama.
Chini yake alikuwepo ‘Echege’ aliyemsaidia Abuna katika mambo ya utamaduni na desturi mahalia. Hata hivyo, kiongozi halisi wa Kanisa hilo alikuwa ni ‘Negus Negasti,’ ikimaanisha ‘Mfalme wa Wafalme’. Hii iliendelea mpaka wakati wa Negus Haile Sellasie katika karne ya 20.
Malkia Helena akishikilia kama mlezi kwa ajili ya mtoto wake mdogo Negus Lebna Dengel, upinzani wa dola za Kiislamu za Kisomali uliongezeka kwa vita vikali, naye aliomba msaada kwa Wareno. Mjumbe Mreno alipofika kukagua alikuta mfalme Lebna Dengel (1508-40) amekimbilia milimani, na nchi yake imeharibiwa na Wasomali wa Haral chini ya Ahmedi Ihn Ibrahim, wakisaidiwa na bunduki za Waturuki.
Mwaka 1543 Wareno walituma askari 400 wenye bunduki wakawashinda Wasomali, Ahmedi akauawa vitani. Hii ilinusuru ufalme wa Ethiopia na kufungua uhusiano na nchi za nje. Hapo kinaishia kipindi cha kwanza ambapo Ethiopia ilikuwa imefungwa bila uhusiano na nchi za nje za Kikristu.