Dar es Salaam
Na Edvesta Tarimo
Kwa mujibu wa Benki ya Dunia (World Bank -2023), inakadiriwa kuwa uzalishaji wa taka utaongezeka kwa 70% kutoka tani bilioni 2.01 hadi bilioni 3.40 ifikapo mwaka 2050.
Kulingana na ripoti ya taarifa ya kiuchumi ya Urejelezaji wa Marekani
(U.S Recycling Economic Information - REI), San Francisco, Marekani, ni jiji la kijani kibichi hasa, na linatajwa kama kinara kwa urejeshaji wa taka (recycling), kwa zaidi ya asilimia 80 ya taka zake.
Urejelezaji wa taka na mifumo mizuri ya kushughulika na majitaka, utasaidia kuongeza ajira, kuongeza viwanda vidogo vidogo, kuongeza teknolojia mpya, pamoja na kipato ambacho kimekuwa kikipotea, ikiwa ni pamoja na kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa.
Majiji mengine yanayofanya vizuri kwenye urejeshaji wa takataka ni pamoja na Curitiba - Brazil, iliyofanikiwa kwa asilimia 70, pamoja na Vancouver-Canada, waliofanikiwa kwa asilimia 60 wakiwa na lengo la kufikia asilimia 100 ifikapo mwaka 2040.
Wanafanyaje? Kwa kushikamana na mipango madhubuti ya kuchakata taka na sera ya kulipa fedha kadri wakazi wake wanavyotupa taka zisizoweza kutumika tena, huwafanya wananchi wawe na ufahamu zaidi wa mazingira, hasa kuhusu bidhaa wanazonunua katika kuepuka kulipishwa fedha zaidi za taka.
Nini kifanyike kukabiliana na hili?
Jiji la Dar es salaam ambalo linatajwa kuwa kitovu cha biashara, lenyewe linakadiriwa kuzalisha zaidi ya tani 4,252 za taka kwa siku moja. Kati ya taka hizo, ni asilimia 50 tu ndizo zinazopokelewa kwenye maeneo maalumu, nyingine zikisalia na kutupwa kwenye mitaro, maeneo ya wazi, na hata barabarani.
Hapa Tanzania, baadhi ya wadau wa mazingira wamekuja na mpango mkakati wa kuweka mazingira katika hali safi kwa kukusanya takataka, na kwa kupita baadhi ya masoko katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kama vile Ilala, Buguruni. n.k.
Alpha Ntibachunya ameamua kushiriki katika utunzaji wa mazingira kwa kuanzisha kampuni ya LIMA ya kurejeleza taka ngumu katika matumizi mengine, badala ya kutupwa na kuchafua mazingira.
Ntibachunya anasema kuwa yeye na mwenzake walifanya utafiti wa kujua takataka zinazotupwa zinapelekwa wapi baada ya kukusanywa, na baada ya utafiti, waligundua kuwa kuna fursa nyingi zinazopatikana kwenye takataka.
“Kilichotupelekea tukaanzisha huu mradi, tulikaa tukafanya utafiti na kugundua kwamba kuna changamoto, baada ya hapo tukapata wazo linguine, tukaja na wazo hili la kuzalisha chakula cha kulishia mifugo, na mbolea ambayo tulitazama zaidi wakulima wadogo, hasa wa vijijini,” anasema Ntibachunya.
Anaongeza kusema kuwa njia mbili tofauti wanazotumia katika kukusanya taka, kwa kwenda sokoni, mfano soko la matunda Buguruni, hotelini na kutumia njia ya boksi hai ambalo hupeleka majumbani mwa watu kwa ajili ya kukusanyia mabaki ya vyakula majumbani mwa watu, kisha wanakwenda kuzichukua na kwenda kuzichakata.
Anasema kuwa wametumia changamoto ya mlundikano wa takataka katika maeneo tofauti tofauti katika jiji kugeuza kuwa sehemu ya kujipatia ajira, na kuajiri vijana wengine katika kukusanya na kuzichakata na kuwa chakula cha kulishia mifugo, na mbolea ambayo ni halisia isiyokuwa na makemiko ya aina yoyote.
Ntibachunya anasema kwamba uchakataji wa taka katika matumizi mengine umekuwa mchango mkubwa wa nafasi ya ajira kwa vijana wengi, kwani uzalishaji wake hauhitaji kiwango cha elimu, bali utayari wa kijana wa kuelekezwa kufanya kazi hiyo.
Kuchakata taka kunanufaisha mazingira, na kunatoa ajira kwa vijana, kunakuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla. Kwa kutenganisha taka zinazoweza kutumika tena kama karatasi, nguo chakavu, glasi, plastiki, aluminium na mabaki ya vyakula na taka za elektroniki, watumiaji wanaweza kusaidia kuunda kijani kibichi kwenye majiji makubwa duniani.
Anitha Erasmi ni mama wa watoto wanne, anasema kuwa uchakataji wa taka umekuwa sehemu yake ya kujipatia kipato cha kuendesha maisha ya familia yake, licha ya ndugu kumwona kama amechanganyikiwa.
“Mwandishi, ndugu zangu na jamii, iliniona kama chizi, lakini mimi sikujali kwa sababu mjini kama huna kazi, ukichagua kazi utashindwa kuishi. Nakusanya mamboga mboga nazipeleka kuziuza, napewa pesa,” anasema Anitha.
Philbert Alphonce mkazi wa Goba jijini Dar es Salaam, anasema kwamba amekuwa anakikusanya taka ngumu kutoka soko na kuzipeleka sehemu wanakozichakata na kuzirejelesha katika matumizi ya kulisha baadhi ya mifugo, na pia mbolea asilia ambayo hutumiwa na wakulima wadogo wadogo kuweka kwenye mashamba ya mboga na maua.
Alphonce anasema amekuwa akiendesha familia yake ya mke na watoto wawili kupitia kazi yake ya ukusanyaji wa mabaki ya mbogamboga na kwenda kuziuza, ambapo kwa wiki anakwenda sokoni mara mbili, huku siku nyingine akizitumia kwa shughuli zake nyingine.
NEMC,Wadau watoa neno
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (National Environment Management Council – NEMC), Dk. immaculate Sware Semesi anasema NEMC, na taasisi ya mazingira, kituo cha Sayansi cha Mazingira (Centre for Science and Environment - CSE), kutoka India, wamekutana nchini Tanzania kujenga uelewa wa nini kifanyike katika taka ngumu, kuchukua takwimu ni taka kiasi gani zinazalishwa na zinatunzwaje, ili ziwe fursa badala ya kuwa uchafuzi wa mazingira.
Dk.Semesi anasema sambamba na hilo, kutambua ni teknolojia gani itumike ili kufanya taka zisiwe kero katika manispaa na jiji, bali ziwe fursa ya kuzalisha ajira au nishati kutokana na taka.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila katika moja ya hotuba yake alisema kwamba anaiona fursa kubwa kwenye wingi wa taka hizo, na tayari alisafiri mara moja kwenda kwenye jiji la Bursan nchini Korea Kusini kujifunza namna wenzetu walivyofanikiwa kwenye urejelezaji wa taka, na kuzifungamanisha na fursa kwa vijana wa rika mbalimbali.
Chalamila anasema kwamba jiji la Dar es salaam linaweza kuwa mfano kwa majiji mengine nchini Tanzania na Afrika Mashariki kwa fursa ya ajira kwa njia ya urejeleshaji wa taka, endapo juhudi za makusudi zitachukuliwa na kufanyiwa kazi kwa vitendo.
Anaongeza kuwa urejelezaji wa taka (recycling) ni mchakato wa kutibu taka kwa lengo la kuokoa malighafi zilizopo ndani ya taka na kuzirejesha kwenye matumizi ya kiuchumi.
Vifaa vya kielektroniki kama simu na kompyuta hurejelezwa na kutumika tena katika kutengeneza matofali, saruji na vyombo vipya vya glasi.
Taka za kaboni kama maganda ya matunda na mbogamboga, zinatumika kutengeneza mbolea na karatasi zikirejelezwa na kutumika kama makasha ya mayai na vifungashio vya bidhaa mbalimbali.
Ripoti ya Benki ya Dunia kuhusu maendeleo ya miji, inaonesha kuwa Afrika huzalisha tani milioni 70 za taka kwa mwaka.
Wakati huu ambapo ongezeko la watu wanaohamia mijini linaongezeka kwa kiasi kikubwa, Benki ya Dunia inasema kuwa kufikia mwaka 2025, uzalishaji wa taka huenda ukafikia tani milioni 160 kwa mwaka.
Tafiti zinasema kwamba ni rahisi kutengeneza bidhaa kutoka nyenzo zilizorejelezwa, kwani bidhaa kama ya aluminium iliyorejelezwa inaweza kuandaliwa tena na kuuzwa kwa bei nusu, kutokana na kuhitajika nishati kidogo ya kuchakata aluminium iliyorejelezwa, kuliko kutumia aluminium mbichi ya kiwandani inayotumika kwa mara ya kwanza.
Urejelezaji pia huepusha gharama ya utupaji wa taka kwenye dampo na vichomaji (incinerators), kwani baada ya kuanza kwa urejelezaji, dampo chache zitahitajika, na ardhi zaidi zilizokuwa zimetengwa kuhifadhi taka huweza kutumika kiuchumi.
Aidha, mapato ni sehemu nyingine aliyoiona Chalamila, kwani urejelezaji huimarisha tasnia ya uchakataji, na hivyo kutengeneza nafasi mpya za kazi kwenye viwanda vidogo vitakavyoundwa, kama viwanda vya chuma, karatasi, glasi, pamoja na ajira kwenye vituo vya ukusanyaji taka, na hata warejeshaji husika.
Utafiti wa U. S Recycling unaonesha kuwa nguvukazi ya kuchakata na kutumia tena malighafi zinazotokana na taka, imekuwa kubwa zaidi kwenye mataifa mengi, zaidi ya nguvukazi inayotumika kwenye uchimbaji wa madini na usimamizi wa taka zisizorejelezwa.Mashirika yanayorejeleza taka, huzalisha takribani dola bilioni 240 kwenye mapato ya kila mwaka.
Huko Carolina kusini pekee, zaidi ya wafanyakazi 15,000 na dola za Marekani milioni 69 za ushuru, hutokana na uchakataji wa taka, huku Carlifonia urejelezaji wa taka ukiajiri watu 85,000.
Kila mwaka, dunia inageuka kuwa makao ya takribani tani bilioni 2.01 za taka ngumu, na idadi hiyo inatarajiwa kufikia bilioni 3.40 miaka 30 ijayo, sawa na ongezeko la 70%.
Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, (World Bank – WB), mataifa yenye kipato cha juu inaonesha kwa siku kuna ongezeko la 19%, huku mataifa yenye uchumi wa kati na chini, ukiongezeka kwa 40% au zaidi.