Dar es Salaam
Na Mwandishi wetu
Paroko Msaidizi wa Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Kalmeri, Bunju, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Paul Mallewa, amesema kuwa Yesu akijitoa sadaka kwa ajili ya ukombozi, akiwasihi waamini kujisadaka na wao ili kuitangaza Injili yake Mwokozi.
Padri Mallewa alisema hayo wakati akitoa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Ekaristi Takatifu, iliyofanyika hivi karibuni parokiani hapo.
“Yesu amejitoa sadaka, nasi tunapaswa kujitoa sadaka kwa ajili ya changamoto katika maisha,”alisema Padri Mallewa.
Alisema kuwa Yesu aliulizwa na wanafunzi wake, ni wapi angependa wamuandalie ale Pasaka, lakini aliwatuma wanafunzi wawili akawambia waende wakakutana na kitu si cha kawaida, hasa kwa wanaume kubeba maji, enzi hizo ilikuwa jambo la kushangaza, kwani kazi hiyo ilikuwa ya wanawake.
“Katika maisha ya kawaida tunakuwa tumebeba mizigo mikubwa, isiyo ya kawaida…Waamini wa Bunju tunapaswa kujitoa kwa dhati, ili tuweze kula Pasaka na Yesu katika majitoleo yetu tunayotoa katika familia zetu,”alisema Padri Mallewa.
Alisema pia kuwa moja ya pasaka ya kula ya Yesu ni kujitoa kwa dhati kuchangia shughuli za Kanisa, kusudi Kristo mwenyewe abadilishe matoleo hayo na kuwa kama sadaka, kama ambavyo yeye alijitoa sadaka ili kuwakomboa wanadamu.
“Yeye ataibadilisha sadaka yetu na kuiweka katika mazingira yasiyo ya kawaida, na kuiweka katika sadaka ya mwili wake, ndipo na sisi tutabarikiwa,”aliongeza kusema Padri Mallewa.
Alibainisha pia kuwa Yesu, pia alitoa damu yake, yenye harufu nzuri ya upatanisho, na utakaso, ambayo inawaimarisha wanadamu wote, hasa wenye changamoto dhidi ya jirani zao na hata kuwa mbali na Kristo mwenyewe.
“Damu ya Kristo Yesu ina harufu nzuri ya upatanisho, harufu nzuri ya msamaha na kuoshwa dhambi zetu na kurudishwa katka hali ya kawaida, damu ambayo tuliipoteza kwa dhambi zetu,” alisema Padri Mallewa.
Naye Paroko wa Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Kalmeri, Bunju, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Dominic Somola, alisema kuwa Pentekoste ni Utatu Mtakatifu, Mwili na Damu ya Bwana Yesu Kristo ambayo ni chimbuko la Kanisa.
Mkakati wa kukuza Watoto Kiimani
Padri Somola alisema kuwa kwa sasa Parokia hiyo ina mikakati mbalimbali ya kuendelea kutoa mafundisho, kwa watoto wadogo, hasa baada ya kupokea Sakranenti, kwani wengi hawafiki kwenda kusali, hasa baada ya kumalizia Masakramenti yao ya awali.
“Wazazi wapo wajitahidi kusimamia imani, kwani ni eneo mtambuka la malezi ya watoto. Sisi kama Parokia, tunajipanga kuhakikisha watoto wanaendelea na mafundisho baada ya kupata Masakramenti yao ya awali,”alisema Padri Somola.
Aidha, Padri Somola alitumia nafasi hiyo kuvishukuru Vyama vya Kitume, Kamati za Liturujia ngazi ya Parokia, kwa kufanikisha siku hiyo ya Ekaristi Takatifu.
Aliwapongeza watoto wote kwa kufanya vizuri mitihani yao ya mafundisho ya Kanisa, na hata wale ambao walifanya vibaya, aliwapa nafasi ikiwemo ya kuendelea kujifunza zaidi, Neno la Mungu.