DAR ES SALAAM
Na Mathayo Kijazi
Vijana wameonywa kuacha kuiga tamaduni zisizofaa, ikiwemo wanaume kuvaa hereni na kusuka nywele zao.
Aidha, wametakiwa kudumu katika imani, wakitambua kwamba tamaduni hizo zinaweza kuwaingiza kwenye dhambi.
Kauli hiyo ilitolewa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu wakati wa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Sakramenti ya Kipaimara kwa vijana 98 katika Parokia ya Mtakatifu Fransisko Ksaveri – Chang’ombe, jimboni humo.
“Mnapopokea Sakramenti hii ya Kipaimara na mnatakiwa muendelee kudumu katika imani yenu, hivyo mnatakiwa kuepuka kuiga tamaduni zisizofaa, mfano, unamkuta mwanaume anavaa suruali anaweka mlegezo, anavaa hereni, anasuka nywele kichwani kama mwanamke. Epukeni kuiga tamaduni za namna hiyo,” alisema Askofu Mchamungu.
Pia, aliwasisitiza kujiepusha na tabia za udokozi pamoja na kutumia mali zisizokuwa za kwao, bali wahakikishe kwamba pale wanapookota vitu, wavirudishe kwa wenyewe.
Aliwasisitiza pia kuwajibika katika usafi pamoja na kutunza mazingira, akisema kuwa suala la usafi wa mazingira wao kama vijana, linatakiwa kuwa kipaumbele kwao.
Wakati huo huo Askofu Mchamungu aliwakumbusha Wasimamizi wa Waimarishwa hao kwamba miongoni mwa majukumu yao, ni pamoja na kusaidiana na Wazazi katika malezi, ili kujenga maadili ya vijana hao.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia hiyo, Padri Novatus Mbaula alimshukuru Askofu Mchamungu kwa kufika parokiani hapo pamoja na kuwaimarisha vijana 98 wa Parokia hiyo.
Aidha, Padri Mbaula aliwasihi vijana hao kuendelea kuyazingatia yale yote waliyoambiwa na Askofu wakati wa homilia yake, kwani mafundisho hayo yatawasaidia kukua katika misingi iliyo bora.
Naye Katibu wa Parokia hiyo, Simon Sangawe alivishukuru vyombo vya habari vya Kanisa vilivyoshiriki katika Adhimisho hilo, ikiwemo Tumaini Media, akisema kuwa vyombo hivyo vinafanya kazi kubwa katika suala la uinjilishaji.