DAR ES SALAAM
Na Mwandishi wetu
Wakatoliki wametakiwa kumtangaza Bwana Yesu Kristo mahali popote, bila uwoga sehemu yoyote na bila kujali jambo lolote na kuacha tabia ya kusaka miujiza.
Wito huo ulitolewa hivi karibuni na Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Ambrosi IPTL, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Paul Sabuni katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika, iliyofanyika katika Parokia Teule ya Utatu Mtakatifu Skaska, IPTL –Salasala jimboni humo.
“Mkristo yeyote inampasa kumtangaza Kristo popote pale anapokuwepo bila uwoga, kwani hiyo ni njia bora zaidi katika maisha yenu ya kila siku,”alisema Padri Sabuni.
Alisema pia kuwa Waamini wa Parokia hiyo Teule wanatakiwa kuwa na Imani thabiti, isiyo suasua hasa katika kuitangaza Injili.
Aliendelea kusema kwamba watu wengi sasa wamekuwa waoga kuzungumza habari za Yesu Kristo, hata kufundisha habari njema.
“Msije mkatetereka kwa kumwogopa mtu yeyote, kwani mkifanya hivyo mtakuwa mmetenda dhambi kubwa ya makusudi kabisa, kutokana na uwoga ndani mwenu wa kumtangaza Kristo,”alisema Padri Sabuni.
Awakanya wasaka miujiza:
Aidha Padri Sabuni, alisema kuwa watu wengi wamekuwa wakitangatanga, kutafuta miujiza na kujikuta wakiingia katika sehemu zisizofaa.
Alibainisha kwamba watu wanaopenda miujiza ni watu wenye imani ndogo, akiwasihi Wakatoliki kuishika imani yao.
“Yesu Kristo alisema kwamba katika siku za mbeleni watakuja manabii wengi wa uwongo,basi inawapasa mtambue kwamba ndio hao wanaowatangazia miujiza kwa sasa,”alisema.
“Inawapasa kushika Imani moja ya Kanisa Katoliki, ambalo lina miujiza, imani kamilifu na muachane na kutangatanga katika madhehebu tofauti, mkifanya hivyo, wewe kama Mkatoliki unamkata Yesu Kristu,”alisema Padri Sabuni.
Padri sabuni pia aliwaomba Waamini wa Parokia hiyo kuchangia Tumaini Media ambayo ina vyombo vitatu navyo ni televisheni Tumaini Radio Tumaini pamoja na gazeti la Tumaini Letu ili Kituo hicho kiweze kupanua wigo wake katika Uinjilishaji.