DAR ES SALAAM
Na Mathayo Kijazi
Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini chini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (Tanzania Episcopal Conference: TEC), wanmekutana katika Mkutano wao Mkuu, huku changamoto za kichungaji, ikiwemo kumomonyoka kwa maadili, zikichukua mjadala mkubwa.
Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Tabora, Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa, amesema kuwa ni vyema kutafakari vema, kama yote yanayoigwa katika Ulimwengu, yanastahili kuigwa ili kuenenda Kiibada na Kiliturujia.
Kardinali Rugambwa alisema hayo wakati akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Maaskofu, uliojadili mambo mbalimbali yanayolihusu Kanisa, Mada kuu ikiwa ni ‘Kuchagiza Hatima ya Waamini Wakatoliki: Changamoto ya Kichungaji katika Maadhimisho ya Miaka 60 ya Lumen Gentium (Mwanga wa Mataifa), uliofanyika Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Kurasini jijini Dar es Salaam.
“Ukitazama baadhi ya mambo yanayoendelea katika Ulimwengu huu, utaona kuwa ni mengi sana. Kwa hiyo tutafakari kwamba, je, yote yanayoigwa katika ulimwengu huu, yanastahili kuigwa ili kuenenda Kiibada na Kiliturujia?
Binadamu wahama misingi ya Imani:
Akizungumzia juu ya mada hiyo kuhusu Changamoto ya Kichungaji katika Maadhimisho ya Miaka 60 ya Lumen Gentium (Mwanga wa Mataifa), Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Mhashamu Isaac Amani, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kurugenzi ya Kichungaji, alisema kuwa binadamu wengi wamehama katika misingi ya kiimani, jambo linalosababisha machafuko na ukosefu wa hali ya amani.
Askofu Amani alisema kwamba uwepo wa Watakatifu, ni mwaliko mama, ambao kila mmoja anatakiwa kuufuata ili kuleta tunu ya kiulimwengu.
Wazazi chanzo kubomoka maadili:
Naye Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu, akichangia mada kuhusu changamoto hizo, alisema kuwa wazazi wanachangia kwa namna fulani watoto kutokuwa na maadili, kwani hawana muda wa kutosha kukaa nao na kujua tabia zao.
“Wazazi wengi hawana muda wa kukaa na kufuatilia mwenendo na tabia za watoto wao, kwa sababu utaona wazazi wanatoka alfajiri kwenda kazini kabla watoto hawajaamka, halafu wanarudi usiku sana, muda ambao watoto wameshalala,” alisema Askofu Mchamungu.
Usafirishaji haramu Binadamu mwiba:
Naye Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi aliwataka wananchi wanaokwenda kufanya kazi katika Mataifa ya mbali kuwa makini, kwani wengi huambulia manyanyaso wanapofika katika Mataifa hayo.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi alitoa rai hiyo wakati akichangia mada kuhusu nini kifanyike, katika kupunguza changamoto zinazowakumba watu mbalimbali, hasa suala la biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu.
“Mwezi uliopita nilisafiri kwenda Adis Ababa, Ethiopia, nilipofika kwenye ndege, nikakutana na wanawake ambao nao walikuwa wanasafiri, nikawauliza ‘mnakwenda wapi?’ wakajibu ‘Muscat’, walisema kwamba wametafutiwa kazi huko wanakwenda kufanya;
“Mimi nikawaambia ‘kuweni makini na hizo kazi mlizoitiwa huko, na mkifika huko msikubali kumpa mtu yeyote Passports zenu, kwa sababu mkiwapa watu Passports zenu, mkifanyiwa jambo baya hamtaweza hata kutoroka,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
Kwa upande wake Sista Digna Chuwa -CPS, Mratibu wa Mradi wa Taasisi ya TCAS, aliyetoa mada ya usafirishaji wa binadamu, alisema kuwa ipo haja ya kushirikiana na jamii kuzuia biashara haramu ya usafirishaji binadamu, kwani hali hiyo huanzia katika familia.
Vyombo vya Kanisa kunasua mtanziko:
Akichangia kuhusu nini kifanyike, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Stephano Musomba alisema kuwa vyombo vya habari vya Kanisa, ni vyema vikatumika ipasavyo, kuandaa vipindi vitakavyosaidia kutoa mafundisho ya imani.
Askofu Kilaini agusia Mtaguso:
Kwa upande wake Askofu Mstaafu wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Mhashamu Method Kilaini alisema kuwa lengo la kuwepo na Mtaguso ni kwenda na wakati, na kuweka vizuri Kanisa kuwa na usawa.
Aliongeza kuwa miongoni mwa malengo hayo, ni pamoja na kutengeneza umoja na kuunganisha urika wa Kanisa zima, mambo ambayo yalichagizwa na Baba Mtakatifu kwa ajili ya kuleta amani ndani ya Kanisa.
Akitoa neno la kufunga Mkutano huo wa Maaskofu, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania,aliyemaliza muda wake, Mhashamu Gervas Nyaisonga, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya, aliwashukuru wote walioshiriki mkutano huo, akisema kwamba anaamini kwamba yote yaliyojadiliwa, yatakuwa msaada katika suala zima la Kichungaji.