DAR ES SALAAM
Na Mathayo Kijazi
Imeelezwa kuwa hakuna kitu kinachoweza kufanywa na Waamini katika Parokia, bila kumshirikisha Askofu Mkuu, kwani vitu vyote ni mali ya Jimbo.
Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Stephano Musomba wakati wa homilia yake katika Adhmisho la Misa Takatifu ya Sakramenti Takatifu ya Kipaimara kwa vijana 80 wa Parokia ya Mtakatifu Teresa wa Benedicta wa Msalaba – Msumi, jimboni Dar es Salaam.
“Maeneo yote hayo mliyoyanunua, mjue kwamba ni mali ya Jimbo, sawa jamani. Kwa hiyo, msije mkaanzisha kitu chochote kile, bila kumhusisha Askofu Mkuu, kwa sababu nilisikia tetesi tetesi kwamba mnataka kununua sijui shamba la kuzikia, mkienda kienyeji bila baraka ya Askofu Mkuu, ni kosa,” alisema Askofu Musomba.
Awali, katika homilia yake Askofu huyo aliwataka wazazi kuongeza usimamizi kwa watoto wao waliopokea Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, kwani hiyo itawasaidia watoto hao kutambua wajibu wao walioitiwa.
“Kwa hiyo wazazi na walezi, ni jukumu lenu kuongeza usimamizi kwa watoto hawa kwa sababu hiyo ndiyo njia itakayowafanya watambue wajibu wao. Hakikisheni watoto hawa wasiyumbishwe wala wasichanganywe katika imani,” alisema Askofu Musomba.
Vile vile, alisema kuwa mtoto anapopokea Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, anatakiwa kushuhudia kile anachokiishi, kwani kwa Sakramenti hiyo, tayari ameimarika.
Aliongeza kuwa Sakramenti hiyo Takatifu ina umuhimu mkubwa kwa kila anayeipokea, kwa sababu inamkamilisha katika Neema ya Ubatizo, na kumkamilisha pia katika imani Katoliki.
Sambamba na hayo, Askofu huyo Msaidizi aliwakumbusha Wakristo kutambua kwamba zawadi ya Kristo mfufuka kwa Waamini wake, ni amani.
Wakati huo huo, Askofu huyo, aliwasihi Waamini wa Parokia ya Msumi kumshukuru Mungu, kwani kupitia Adhimisho hilo la Misa Takatifu, wamepata Wakristo wengine 80 waliokomaa ambao ni Waimarishwa.
Aliwashukuru Waamini wa Parokia hiyo kwa kuwachangia Skauti Shilingi laki 3 kwa ajili ya Kongamano lao linalotarajia kufanyika jimboni humo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Parokia hiyo, Frank Werema, katika risala yake, alisema kuwa miongoni mwa mambo wanayoendelea kuyafanya kiroho, ni pamoja na kuwahamasisha Waamini ambao bado hawajafunga ndoa, wafunge, kwani kaya zaidi ya 482, wakazi wake hawajafunga ndoa.
Akizungumzia changamoto zinazowakabili hadi sasa parokiani hapo, Mwenyekiti huyo alisema kwamba kubwa ni ubovu wa miundombinu ya barabara katika maeneo ya Parokia hiyo.
Naye Mwandishi Laura Chrispin, anaripoti kuwa, Watoto wanaopokea Sakramenti Takatifu ya Kipaimara wametakiwa kufahamu kuwa wanampokea Roho Mtakatifu kwa mara ya pili atakayewaongoza siku zote za maisha yao.
Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Stephano Musomba wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Sakramenti Takatifu ya Kipaimara iliyofanyika katika Parokia ya Mtakatifu Martha -Mikocheni, alisema kuwa hata kipindi cha Mitume kabla ya kumpokea Roho Mtakatifu, Mitume mara zote walikuwa ni watu wa kuuliza maswali lakini baada ya kumpokea Roho Mtakatifu, walikuwa ni watu wa ushuhuda zaidi.
Hiyo ikiwa ni kama funzo kwenu kuwa inawapasa kuwa ni watu wa kumshuhudia Kristu kwa matendo yenu wenyewe, pamoja na kueleza makuu ya kristu kwa watu wengine.
Alisema hata katika Sinodi ya Maaskofu, inatuelekeza kutembea pamoja na kuwataka wengine wasibaki nyuma bali kutembea pamoja, ndiyo maana ukisema Kanisa la Kisinodi unaseama Ushirika na Ushiriki wa Kimisionari.
Katika Ushirika hawa ni Wanajumuiya, Wanafamilia ambayo kuna huduma wana hudumiana na kufanya kazi zote kwa pamoja na ni washiriki, ndo mana wanakuwa Wamisionari.
Mhashamu Musomba alisema “Roho Mtakatifu anavyokuja kwetu, anatufanya tuzungumze Lugha moja, hiyo ambayo ni katika upendo zaidi”.
Askofu Musomba aliwataka Waamini kuwa na amani katika familia zao na kumwomba zaidi Mungu awaepushe na dhambi kwani dhambi ni mojawapo ya sababu inayopelekea kupotea kwa amani.
Aidha, aliwataka Waamini kutosahau baadhi ya dhambi, hasa dhambi ya jamii ambayo ni kwa mtu yeyote anaweza kufanya mfano kwa wafanya biashara kutengeneza chakula kwa uchafu na kusababisha magonjwa kwa jamii, hiyo ni dhambi na inakupasa kuiungama mara moja.
Askofu Musomba alitoa wito kwa wazazi na walezi kwa kuwataka wasaidie kuwasindikiza katika imani moja ya Kanisa Katoliki, na siyo kuwachanganya watoto katika imani zingine.