ZOMBA, Malawi
Baba Mtakatifu Fransisko amemteua Padri Alfred Mateyu Chaima kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Zomba, nchini Malawi.
Baraza la Maaskofu Katoliki wa Malawi (Episcopal Conference of Malawi: ECM) lilithibitisha uteuzi huo katika taarifa yake iliyotiwa saini na Rais wake, Askofu Mkuu George Desmond Tambala, ikieleza kuwa hiyo ni katika kutekeleza kazi ya Mungu.
“Naomba kila mmoja ajiunge nami, Jimbo la Zomba na Baraza zima la Maaskofu wa Malawi kumpongeza Askofu Mteule. Tumkumbuke katika maombi yetu kwa ajili ya huduma nyenyekevu na yenye mafanikio ya Uaskofu wake. Wema wa Bwana unaendelea kujitokeza mbele yetu,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Jimbo Katoliki la Zomba limekuwa bila Askofu kuanzia Oktoba 2021, kufuatia Askofu wa wakati huo Mhashamu George Desmond Tambala kuteuliwa kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Lilongwe.
Kufuatia hali hiyo, Jimbo Katoliki la Zomba limetangaza kuwa sherehe za kumweka wakfu Askofu huyo, zitafanyika Agosti 12 mwaka huu.
Akijibu habari za uteuzi wake, Padri Chaima alisema kuwa amepokea uteuzi huo na anatambua kuwa si kazi rahisi, akiwaomba watu wenye mapenzi mema, kumkumbuka daima katika sala.
“Nimefurahia maendeleo kama mtumishi katika huduma ya Mungu, ambapo unapaswa kuwa tayari kwenda popote unapoombwa kwenda. Nitategemea maombi yangu pamoja na maombi ya watu wote kanisani ili nifanikiwe,” alisema Askofu Mteule Chaima.
Askofu Mteule Chaima alihudumu kama Katibu Mkuu wa ECM katika Sekretarieti ya Kanisa Katoliki. Mbali na hayo, alihudumu katika nyadhifa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kama mwalimu, Mratibu na Mkuu katika Seminari Ndogo ya Pius XII; na Katibu wa Kichungaji wa Jimbo Kuu la Blantyre.
Alikuwa Mkurugenzi wa Nantipwiri Pastoral Centre, Mwenyekiti wa Bodi ya Chama cha Kikristo cha Afya (CHAM), Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Malawi, na Mhadhiri wa Muda katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Malawi - Idara za Theolojia na Mafunzo ya Dini/ Biblia na mhadhiri wa muda katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki, Chuo cha Tangaza na Taasisi ya Kichungaji ya Gaba, kwa kutaja machache tu.
Safari yake ya Upadri ilianzia katika Seminari ya Mtakatifu Pius XII ambako alipata elimu ya sekondari, na baadaye alijiunga na Seminari Kuu ya Kachebere kwa masomo ya Falsafa, na kisha aliendelea na masomo ya Theolojia katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Petro huko Zomba.
Alipewa Daraja ya Ushemasi mwaka 1998 katika Kanisa Kuu Katoliki la Zomba, Jimbo Kuu Katoliki la Zomba, na baadaye akawa Kuhani katika Kanisa Kuu la Limbe, Jimbo Kuu Katoliki la Blantyre mwaka 1998.
Ana Shahada ya Udaktari (PhD) katika Theolojia ya Kichungaji kutoka Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki (Catholic University of Eastern Africa: CUEA).