DAR ES SALAAM
Na Mathayo Kijazi
Wakati Mfungo wa Kwaresma ukiwa umeanza, Wakristo wametakiwa kujikita katika toba, sala, kufanya matendo ya huruma na upendo katika kipindi chote cha mfungo huo wa siku 40.
Wito huo ulitolewa na Maaskofu, na Mapadri wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam wakati wakitoa homilia katika Maadhimisho ya Misa Takatifu zilizoadhimishwa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu; Parokia ya Mtakatifu Petro – Oysterbay; Parokia ya Mwenyeheri Isdori Bakanja – Boko; na Parokia ya Kristo Mfalme – Tabata.
Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, aliyeadhimisha Misa Takatifu katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu, alisema kuwa ni vyema kujikita katika matendo ya huruma na upendo, huku wakimrudia Mungu.
“Ndugu zangu, Neno la Mungu kwa msisitizo mkubwa, litatualika na kutuasa kujikita katika toba, kujikita katika sala, kujikita katika huruma na upendo tukimrudia Mungu. Hizi ni zama za mtandao. Kishawishi kikubwa, ni kule watu kutaka kufanya mambo yaonekane mtandaoni,” alisema Askofu Mkuu.
Askofu Mkuu alisema kuwa toba ya kweli siyo mambo ya mtandao, bali ni mabadiliko ya ndani, kuongoka rohoni, kumrudia Mungu kwa dhati, pamoja na kuanza upya, kwani hilo ndilo waliloaswa katika masomo waliyoyapitia katika Misa hiyo.
Pia, aliwasisitiza Waamini kufahamu kwamba majivu ni kielelezo cha toba, akisema kuwa watu wa kale walipofanya toba, walijipaka majivu, wakajivika magunia, na wakatembea katika unyofu na uadilifu.
Aliongeza kuwa Wakristo wanapopakwa majivu na kufanya toba, hawatakiwi kufanya maonyesho, bali wamwombe Mungu kwa mioyo radhi ili awahurumie dhambi zao, awajaze neema yake, na awajalie wajikite katika safari ya kipindi cha Kwaresma, huku wakimrudia Mungu.
“Sisi tunapojipaka majivu tukifanya toba, hatutaki kufanya maonyesho, bali tunataka kumwomba Mungu kwa mioyo radhi, atuhurumie dhambi zetu, atujaze neema yake, atujalie tujikite katika safari ya kipindi cha Kwaresma, tumrudie Mungu tukimwomba toba kwa ajili ya dhambi zetu, kwa ajili ya dhambi za ulimwengu, na yote yale yaliyo machukizo kwake.
Kwa upande wake Askofu Msaidizi wa Jimbo hilo, Mhashamu Stephano Musomba wakati wa homilia yake katika Parokia ya Mtakatifu Petro – Oysterbay jimboni humo, aliwataka Wakristo kuwa wanyenyekevu, huku wakitambua mipaka yao, udhaifu wao, na kufahamu kwamba Mungu ni muhimu katika maisha yao.
Katika homilia yake, Askofu Msaidizi Musomba aliwataka Waamini katika kipindi hiki cha Kwaresma, kuombana msamaha pale wanapokoseana, na pale wanapomkosea Mungu, ili waanze upya na waendelee vizuri na maisha yao.
Naye Paroko wa Parokia ya Mwenyeheri Isdori Bakanja – Boko, jimboni humo, Padri Emmanuel Makusaro aliwaalika Waamini kufunga matendo ya dhambi pamoja na kuwasaidia wahitaji, kwani hapo Kwaresma ndipo itakuwa na nguvu zaidi.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia ya Kristo Mfalme – Tabata, jimboni humo, Padri Cornelius Mashare alitoa wito kwa Waamini kutafakari, huku wakiishi maisha ya unyenyekevu na yenye kumpendeza Mungu katika kipindi hiki cha Kwaresma.