DODOMA
Na Bartholomew Wandi
Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 hauko mbali sana kuanzia sasa, kwani ukipiga hesabu umebaki takribani muda wa mwaka mmoja (1) na miezi kadhaa hivi. Wananchi wengi ambao watafikisha miaka kumi na minane wakati wa jukumu hili, waliofikisha miaka kumi na minane (18) tayari na zaidi, na wale ambao waliokuwa na sifa zote za kuandikishwa mwaka 2020, lakini kutokana na sababu zisizoweza kuzuilika walikosa nafasi ya kuandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, wataandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwenye Awamu ya Kwanza na ya pili ya uboreshaji.
Mpaka sasa mikoa yote 25 Tanzania Bara tayari ina watu ambao wanahitaji kuandikishwa kuwa wapiga kura wenye sifa nilizozielezea hapo juu.Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ni hitaji la kisheria na Kikatiba pia. Tume ya Taifa ya Uchaguzi, imepewa jukumu la kisheria kuandikisha wapiga kura katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kuliboresha Daftari hilo kwa ajili ya Uchaguzi wa Rais na Wabunge wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania na pia Madiwani Tanzania Bara.
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utakuwa mahsusi kwa ajili ya kuandikisha wapiga kura wapya, wanaohitaji kurekebisha taarifa zao zilizokosewa awali, waliopoteza kadi za kupigia kura, wenye kadi zilizoharibika ili waweze kupata kadi nyingine, na wale ambao wanataka kuhama Jimbo au Kata kwenda Jimbo au Kata nyingine ili waweze kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Kifungu cha 12 (2) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024 inaeleza, “Mkurugenzi wa Uchaguzi ataweka, atatunza na kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lililoanzishwa chini ya kifungu cha (1)”.
Kulingana na Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, Kifungu cha 9 (2) inasema, “Bila kujali Masharti ya kifungu kidogo cha (1), na kwa kuzingatia uthibitisho wa umri , Mtanzania yeyote ambaye hajapoteza sifa chini ya Sheria hii au Sheria nyingine yoyote ya Bunge, na ambaye wakati au kabla ya tarehe ya Uchaguzi atatimiza umri wa miaka kumi na minane (18) atastahili kuandikishwa kuwa Mpiga Kura chini ya
Kifungu cha 13 (2) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, pia inaeleza kwamba, “Tume itamwandikisha mtu yeyote Tanzania Zanzibar ambaye anastahili kuandikishwa kuwa mpiga kura katika Uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano”.
Zaidi ya hayo, Ibara ya 5(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, inafafanua, “Kila raia wa Tanzania aliyetimiza umri wa miaka kumi na minane (18) anayo haki ya kupiga kura katika uchaguzi unaofanywa Tanzania na wananchi. Na haki hii itatumiwa kwa kufuata masharti ya ibara ndogo ya (2) pamoja na masharti mengine ya Katiba hii na ya Sheria inayotumika nchini Tanzania kuhusu mambo ya uchaguzi”.
Pamoja na hayo, pia Ibara ya 5(3)(a-d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, inaeleza kuwa Bunge litatunga sheria ya uchaguzi na kuweka masharti kuhusu kuanzisha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kuweka utaratibu wa kurekebisha yaliyomo katika Daftari hilo, kutaja sehemu na nyakati za kuandikisha wapiga kura na kupiga kura, utaratibu wa kumwezesha mpiga kura aliyejiandikishwa sehemu moja kupiga kura sehemu nyingine na kutaja masharti ya utekelezaji wa utaratibu huo, na kutaja kazi na shughuli za Tume ya Uchaguzi na utaratibu wa kila uchaguzi ambao utaendeshwa chini ya uongozi na usimamizi wa Tume ya Uchaguzi.
Marekebisho ambayo yanapaswa kuingizwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ni kuondoa wapiga kura waliojiandikisha zaidi ya mara moja, waliojiandikisha na huku wako chini ya umri wa miaka kumi na minane (18), waliofariki dunia au kupoteza sifa ya kuwa wapiga kura kwa namna nyingine, kuwapa kadi za mpiga kura mpya waliopoteza kadi zao, kurekebisha taarifa za wapiga kura zilizokosewa awali, na kuwaingiza waliofikisha umri wa miaka kumi na minane (18) na kuendelea.
Kifungu cha 16(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024 inasema, “Tume itakuwa na jukumu la kupanga muda na kupitia upya uandikishaji wa wapiga kura katika kila eneo la uchaguzi ndani ya jimbo”
Kwa mujibu wa kifungu cha 16 (5) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, inaeleza kwamba Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utafanyika mara mbili kwa miaka mitano (5), yaani baada ya Uchaguzi Mkuu kupita, na kabla ya siku ya uteuzi.
Uchaguzi Mkuu wa Mwisho ulifanyika Oktoba 28 mwaka, 2020, na sasa Tume ipo kwenye maandalizi ya kuboresha Daftari hilo kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025. Mchakato wa Uboreshaji huo wa Daftari umeanza kwa kukagua vituo vilivyotumika kuandikishia Wapiga Kura mwaka 2019/2020.
Uhakiki huo wa vituo hivyo vya kuandikishia wapiga kura, unalenga kuona kama kuna haja ya kuongeza vituo, kuona kama vilivyopo bado vinakidhi matakwa ya kisheria, na kufanya marekebisho mengine kama vile kubadilisha au kurekebisha majina ya vituo vilivyokosewa.
Matokeo ya uhakiki huo kwa Tanzania Bara yanaonesha kuwa, vituo vya kuandikisha wapiga kura vimeongezeka kutoka 37,814 hadi 40,126 ambapo kati ya vituo hivyo, 39,709 ni vya Tanzania Bara na vituo 417 ni vya Zanzibar.
Baada ya kazi ya kukagua vituo hivyo, Tume imefanya Uboreshaji wa majaribio (pilot) unaofanyika katika baadhi ya vituo vilivyoko kwenye halmashauri za Wilaya na Halmashauri za miji kwa lengo la kujaribu kuona namna na jinsi vifaa vya uboreshaji vinavyofanya kazi katika mazingira tofauti, na kupata namna bora ya kufanikisha zoezi hili la uboreshaji.
Tume tayari imeshafanya uboreshaji wa majaribio katika kata ya Ikoma iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Rorya Mkoani Mara na Kata ya Ng’ambo iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora Mkoani Tabora. Kata hizi zilichaguliwa ili kupata mazingira tofauti ya kijiografia, pamoja na idadi ya watu.
Uboreshaji huu wa majaribio umefanyika kwa mafanikio kutokana na kuboreshwa kwa vipuri na mfumo wa uandikishaji wa wapiga kura. Aidha, ilibainika kuwa betri mpya za BVR Kits zinao uwezo wa kuhifadhi chaji kwa muda mrefu, na hivyo zitaweza kukabiliana na changamoto ya nishati ya umeme katika baadhi ya maeneo ambayo hayana miundo mbinu hiyo.
Pamoja na mafanikio hayo kulikuwa na changamoto ndogo ya baadhi ya wapiga kura kutokuwa na uhakika ama kukumbuka majina yao wanapokuja kurekebisha taarifa zao na hivyo kuchukua muda mrefu kituoni kutokana na kazi ya kutafuta majina yao kwa usahihi. Tume ya Taifa ya Uchaguzi itaendelea kuwaelekeza Wapiga Kura kuhakikisha wanakumbuka taarifa zao kwa usahihi ili waweze kuhudumiwa kwa haraka vituoni.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jacobs Mwambegele wakati akiongea na Waandishi wa Habari Mjini unguja, Zanzibar, amesema kuwa uzinduzi rasmi wa Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utafanyika Mkoa wa Kigoma tarehe 01 Julai, 2024.
Uboreshaji huo wa Daftari kwa Teknolojia ya BVR kwa mwaka huu 2024, hautakuwa tofauti na wa mwaka 2019/2020, ambao ulihusisha wananchi wote wapya wenye sifa za kuwa wapiga kura, waliohama jimbo au Kata, na ambao kadi zao zilipotea au kuharibika.
Wapiga kura ambao waliandikishwa mwaka 2015 na 2020 na wanazo kadi zao za kupigia kura na hazina matatizo yoyote, au hawajahama Jimbo/Kata kwenda Jimbo/Kata nyingine au hakuna mabadiliko yoyote ya mipaka ya kiutawala, wanatakiwa pia kwenda katika vituo vya kuandikisha Wapiga Kura ili kuhakiki taarifa zao kwenye Daftari.
Kwa upande wa idadi ya Wapiga Kura watakaoandikishwa awamu hii, Tume imeshafanya makadirio kulingana na uandikishaji uliopita pamoja na matokeo ya Sensa ya watu na makazi uliofanyika mwezi wa Agosti mwaka huu, 2022.
Mhe. Jaji Mwambegele aliwaambia Waandishi wa Habari kuwa, makadirio ya Tume kwa kutumia ripoti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ya Sensa ya Watu na Makazi, inatarajiwa idadi ya Wapiga Kura kuongezeka kufikia 34,746,638 kutoka 29,754,699 ya Wapiga Kura katika mwaka 2020, idadi hii itajumuisha wapiga kura wapya 5,586,433, sawa na asilimia 18.7 wanaotarajiwa kuandikishwa.
Pamoja na hayo, Mwnyekiti wa Tume anasema kuwa inakadiriwa Wapiga Kura 594,494 wataondolewa katika Daftari kwa kupoteza sifa na jumla ya Wapiga Kura 4,369,531 wataboresha taarifa zao. Hawa watakaoboresha ni wale ambao taarifa zao zilikosewa au wamehama kutoka Kata au Jimbo moja kwenda eneo lingine la Uchaguzi, na wengine ni wale ambao kadi zao zimeharibika au zimepotea.
Hata hivyo, Uboreshaji wa safari hii hautofautiana sana na ule wa mwaka 2015 na 2020, kwani Teknolojia itakayotumika ni ile ile ya kuchukua alama za kibaiolojia yaani Biometric Voters Registration (BVR), pamoja na Android.
Aidha, mabadililiko yanayotazamiwa ni kwa upande wa kupunguza ukubwa na uzito wa BVR Kits ambapo awali wakati wa uboreshaji wa Dafrari wa mwaka 2014/2015 na 2019/2020 BVR zilikuwa na uzito wa kilo 35 lakini kwa uboreshwaji wa mwaka huu kwa 2024/2025, uzito umepunguzwa hadi kufikia kilo 18 ambapo yapo masanduku mawili, moja ni kwa kuhifadhia mashine ya BVR Kits, na lingine ni kuhifadhia vifaa vingine vya kuunganishia BVR Kit hiyo ikiwemo kishikwambi kwa ajili ya kupigia picha ya Mpiga Kura na kuchukulia alama za vidole, ila vifaa hivi vitatoa huduma ile ile ya kuandikisha wapiga kura na kutoa kadi hapo hapo kituoni.
Mabadiliko mengine katika Uboreshaji wa Daftari ni Tume kuanzisha mchakato wa uboreshaji kwa njia ya mtandao (Online) ambapo mpiga kura anaweza kuanzisha mchakato huu wa awali kwa njia ya mtandao ili kurekebisha, au kubadilisha taarifa zake, kuhamisha taarifa zake kutoka kituo cha awali kwenda kingine, au anayetaka kufanya vyote kwa pamoja.
ITAENDELEA WIKI IJAYO.
Wapiga kura wanaotaka kuboresha taarifa binafsi na wanaohama vituo au vyote viwili kwa wakati mmoja, wanaweza kuanzisha mchakato wa kuboresha taarifa zao kwa njia ya mfumo wa mtandao ‘online’ kuingia kwenye Tovuti ya Tume www.inec.go.tz kwa kutumia kompyuta au simu janja, kisha atabonyeza kiunganishi (link) iliyoandikwa Boresha Taarifa za Mpiga Kura, au atatumia anuani ya ovrs.nec.go.tz itakayompeleka moja kwa moja kuanzisha mchakato huo.
Katika mfumo huu, wapiga kura wanatakiwa kuingiza namba ya kitambulisho cha taifa (National Identity Number: NIN), namba ya kadi ya mpiga kura, namba ya simu anayotumia kwa sasa, na jina la Kata, kisha watapata ujumbe wenye namba za utambulisho (token namber) ambazo wataenda nazo kituoni ili kukamilisha taratibu za kupata kadi za mpiga kura.
Mwombaji ambaye ni mpya anatakiwa kwenda kituoni bila kuwa na kitambulisho cha aina yoyote kiinachomtambulisha ili aweze kupatiwa kadi ya mpiga kura. Mwaombaji huyu atakapofika kituoni atamwona Mwandishi Msidizi wa Kituo cha kuandikisha Wapiga Kura na kuajaza fomu Na. 1,
Baada ya kujaza Fomu Na. 1, Mwombaji huyo Mpya atampatia Afisha Mwendesha Mashine ya Bayometriki (BVR Kits Operetor) ambaye ataingiza taarifa zake kwenye BVR Kit, atapigwa picha, atachukuliwa alama za vidole kumi vya mikono yote miwili na kuweka saini na kupewa Kadi ya Mpiga Kura hapo hapo kituoni.
Kwa wapiga kura ambao walipoteza, kuharibika au kukosewa Kadi zao na ambao hawatajaza Online, watakapofika Kituoni, watajaza fomu Na. 5A kwa Mwandishi Msaidizi wa Kituo , kisha Afisa Mwendesha Mashine ya Bayometriki ataingiza taarifa zao kwenye BVR Kit, akisha watapigwa picha, watachukuliwa alama za vidole kumi vya mikono yote miwili, na kuweka saini na mwishowe watapewa Kadi zao za Mpiga Kura hapo hapo kituoni.
Vile vile,, Wapiga Kura ambao wanataka kuhamisha taarifa zao, pia watajaza fomu Na. 5A kwa Mwandishi Msaidizi wa Kituo ili kuomba kuhamishiwa taarifa zao kwenda Jimbo au Kata na Kituo kingine cha Kupigia Kura wakati wa Uchaguzi Mkuu, na Chaguzi nyingine Ndogo zitakazofuata baada ya Uchaguzi Mkuu kupita.
Aidha, Mtu anatakiwa aende mwenyewe kituoni na anatakiwa kujiandikisha mara moja tu. Ni kosa la jinai kwa mwananchi yeyote kwa makusudi kwenda kituoni na kujiandikisha zaidi ya mara moja. Mwaka 2015, Kwa Mkoa mmoja tu wa Njombe, Kanzi Data hiyo imeweza kung’amua wapiga kura zaidi ya 600 waliojiandikisha zaidi ya mara moja, na walichukuliwa hatua za kisheria.
Kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, kifungu cha 114(1)(b) inaeleza kuwa “kwa kujua au ana sababu ya kuamini kuwa ameandikishwa katika eneo la Uchaguzi anaomba kuandikishwa kinyume na kifungu cha 25, na bila kufichua kwa Msimamizi wa Uchaguzi kujiandikisha kwake kwa awali katika eneo jingine la Uchaguzi atenda kosa na akitiwa hatiani atapaswa kulipa faini isiyopungua shilingi laki moja na isiyozidi shilingi laki tatu au kifungo cha muda usiozidi Miaka miwili au vyote kwa pamoja”.
Baada ya zoezi hili, Tume ya Taifa ya Uchaguzi itaandaa Daftari la Awali la Wapiga Kura na kupelekwa mikoani kwa ajili ya kuwekwa wazi (Display) kwa ajili ya wapiga kura kuangalia kama majina yao yamo kwenye Daftari.
Kama baadhi ya majina hayaonekani, Wapiga Kura watamweleza Mwandishi Msaidizi kutoonekana kwa majina hayo na Mwandishi Msaidizi ataandika majina ya Wapiga kura hao waliokosekana kwenye Daftari la Awali na kisha ataleta orodha hiyo ya Majina Tume kwa ajili ya kuingizwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Pamoja na hayo, dhumuni lingine la Tume kupeleka Daftari la Awali la Wapiga Kura mikoani kwa ajili ya kuwekwa wazi (Display) ni kuwapa fursa Wapiga Kura kuangalia kama kuna majina ya Wapiga Kura walioandikishwa na hawana sifa kisha watawawekea pingamizi kwa kujaza fomu Na. 3B na kumkabidhi Mwandishi Msaidizi fomu hiyo ambaye ataileta Tume kwa ajili ya Wapiga Kura hao ili wafutwe kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kama kweli hawana sifa.
Hata hivyo, Majina hayo yaliyowekewa pingamizi hayafutwi moja kwa moja kwenye Kanzi Data ya Tume badala yake yanahifadhiwa sehemu nyingine kwenye Kanzi Data ili kama mtu huyo ana ushahidi wa kutosha kuwa ana sifa za kutosha kuandikishwa na kubaki kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura anarudishwa mara moja, Machapisho mbalimbali ya Elimu ya Mpiga Kura ya uhamasishaji ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura yatasambazwa nchi nzima ili kuwaelimisha Wapiga Kura kuwa na uelewa na mwamko wa kujiandikisha kwa wingi kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga kura.
Mchapisho hayo pia yanasistiza Wapiga Kura kutunza Kadi zao za kupigia kura na hatimaye kujitokeza kwa wingi kupiga Kura kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2025 utakapowadia na Chaguzi Ndogo zitakazofuata na kila mmoja anatakiwa awe na Kadi yake ya kupigia kura.
Tume pia katika uhamasishaji wake wa Uboreshaji wa Daftari itatumia vyombo mbalimbali vya habari kama Magazeti, Radio kubwa na Radio za Kijamii, TV, INEC TV ONLINE, Tovuti ya Tume na Mitandao ya Kijamii, machapisho yakiwemo mabango, vijitabu na vipepeperushi, gari la Elimu ya Mpiga Kura na kushirikisha wadau kwa kutoa vibali kwa taasisi na asasi za kiraia.
Mwandishi wa Makala haya ni Afisa Habari Mkuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) Simu 0754203015.