TAFAKARI SOMO LA INJILI DOMINIKA YA 19
Amani na Salama!
“Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye, hataona kiu kamwe.” Haya ndiyo maneno ya hitimisho la somo la Injili ya Dominika iliyopita. Yesu anajitambulisha kwa wasikilizaji wake kwa namna ambayo iliwakwaza, ni maneno yaliyoweka imani yao njia panda, na hapa ndipo tunaona wasikilizaji wake ambao Mwinjili anawatambulisha kama “Wayahudi,” walimnung’unikia Yesu kutokana na maneno hayo.
Wayahudi waliamini kuwa na ukweli wote, na ndiyo Torati na Manabii. “Atamlisha mkate wa ufahamu, na kumnywesha maji ya hekima.” (Yoshua bin Sira, 15:3) Hivyo, ndiyo kusema kuwa mkate wa uzima ni Neno la Mungu ambalo Wayahudi waliamini kuwa nalo katika ukamilifu wake, ndiyo Torati na Manabii na Vitabu vingine vya Maandiko Matakatifu.
Kwao ilikuwa ni makwazo makubwa, kwani Yesu leo anajitambulisha kuwa ni Yeye aliye mkate wa uzima wa milele utokao mbinguni, ni kwa kulisikiliza na kulishika Neno lake, kila mwenye njaa na kiu atashibishwa, na hivyo hataona njaa wala kiu tena.
Wayahudi walishindwa kuupokea utambulisho wa Yesu kama chakula cha uzima, na wakabaki kumwona kama mwana wa Yusufu tu, na tena waliyemfahamu vyema hata kazi na ujira wake kuwa ni ule duni kabisa, na zaidi sana hata mama yake pia walimfahamu. Ni watu waliomfahamu vyema na vizuri, na kwa nini basi anajitambulisha na kujifananisha kuwa ni Mungu, ni kutoka mbinguni?
“Wakasema, huyu siye Yesu, mwana wa Yusufu, ambaye twamjua babaye na mamaye? Sasa asemaje huyu, ameshuka kutoka mbinguni?” Na tunasikia manung’uniko haya hawakumwelekezea Yesu, bali yalikuwepo baina yao, miongoni mwao, kati yao wenyewe.
Kunung’unika siyo kitendo kile cha kulalamika tu. Naomba kieleweke, na Mwinjili anakitumia kitenzi hicho kuonesha mkwamo wao wa kiimani, kukwazika na kujikwaa kwao kwa fundisho lenye utambulisho mpya kumhusu Yesu, utambulisho ambao unamfunua Yesu kuwa si tu mwanadamu kweli, bali pia ni Mungu kweli, ametoka kwa Mungu, amekuja kuifunua katika ukamilifu sura halisi ya Mungu. Kwao haikuwa jambo rahisi na lenye kueleweka kuwa kwa njia ya Yesu, hekima ya Mungu imejimwilisha na kukaa kati yao, na kuwa katikati yao. Soma zaidi Tumaini Letu.