MWANZA
Na Paul Mabuga
Maureen Mwanawasa, Mke wa Rais wa zamani wa Zambia, Levy Mwanawasa [2002 – 2008], amefariki Agost 13, 2024, jijini Lusaka nchini humo baada ya kuugua kwa muda mfupi. Kama ulipata nafasi ya kumfahamu, bila shaka utajiuliza kwa nini akina mama huku kwetu wanashindwa kuwashawishi wanaume wanne wao kwenda kanisani hasa baada ya kuonekana mahudhurio yao ni hafifu na yenye kulalamikiwa.
Fikiria mama wa ‘kibongo’ anaweza kumshawishi mume wake, kulipia hadi shilingi elfu 30 ama hata hamsini, kwa ajili ya kusuka nywele ili apendeze, ama anunulie gauni la mtoko la hadi shilingi 60,000/- na kumsaidia marejesho ya mikopo ya kausha damu, lakini anashindwa kumbembeleza mwanaume ahudhurie kanisani, jambo ambalo hata hivyo haligharimu fedha yoyote.
Safari yangu ya kukutana na Maureen Mwanawasa ilianzia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Keneth Kaunda jijini Lusaka, ambapo wakati natoka nje nikiwa miongoni mwa wageni waliowasili, nilipokelewa na mzee mmoja raia wa Tanzania. Nilishangaa baada ya kuwa licha ya mzee huyo kunizidi umri, lakini alipokea begi langu ambalo lilikuwa mzigo wangu pekee, na kunielekeza kwenye gari ndogo tukielekea katikati ya jiji la Lusaka. Juhudi zangu za kukataa mzee huyu kunibebea mzigo ili kulinda mila za Kiafrika, zilizogonga mwamba.
Hapo safari ikawa moja kwa moja hadi katika hoteli ya Pamodzi [yaani pamoja] ambayo baadaye niliambiwa kuna Marais na Wakuu wa Nchi 14 wanalala hapo, na ndiyo maana ulinzi ulikuwa mkali. Nikajisemea kimya kimya, itakuwaje siye kwa mazoea ya kabila letu kwamba ukinywa hata kabia kamoja, unaanza kuimba. Lakini kwa bahati, mratibu wa mambo akaniambia, “Bwana mdogo twende huku.’’ Nikapelekwa hoteli nyungine jirani ambayo nayo ilikuwa kubwa. Hii ilikuwa ni Agosti 15, 2007.
Jioni hiyo kukawa na zoezi ambapo watu wote waliokuwa wanatarajia kuingia katika vikao vya Marais na wakuu wa Nchi katika Jumuiya ya Nchi zilizo Kusini mwa Afrika [SADC], walitakiwa kufika katika kituo maalum, ambapo baada ya kuhakikiwa, walipigwa picha na kupewa Kitambulisho maalum. Hakuna aliyekuwa akiachwa kwenye hatua hii, isipokuwa mabwana wakubwa.
Wakati nimefikia hatua ya kupigwa picha, akaingia mama mmoja aliyevaa kitamaduni, na baadaye nikabaini kuwa ni mmoja wa wafanyakazi katika Ikulu wa King Mswati lll wa Eswatini. Kwa heshima yake na kwamba anatoka katika familia ya kifalme, jambo ambalo inaelekea Wazambia wanalijali, nikaambiwa nimpishe ahudumiwe kwanza yeye. Nikafanya hivyo, na mimi baadaye nikapata kitambulisho changu.
Asubuhi wakati nakwenda kwenye mkutano, ile naingia geti la kwanza, nikakutana na askari ambaye baada ya kutambua kuwa ninatoka Tanzania, akanionesha kitambulisho cha mmoja wa Mawaziri wa huku kwetu ambacho kumeokotwa. Akaniuliza, unamjua huyu na mimi nikamwambia, naam namjua ni mmoja wa mawaziri wetu, na akanionya, mtafute umpe hiki kitambulisho, vinginevyo hataingia humo ndani. Niliifanya kazi hiyo na baadaye kumkabidhi kitambulisho chake.
Wakati wa mapumziko, nilifanikuwa kuwa karibu na aliyekuwa Rais wa Namibia, Hifikipunye Pohamba, jamaa mrefu hivi, baada ya kumsalimia kwa Kiingereza na kuonesha nia ya kufanya naye mahojiano, aliinama na kusoma kutambulisho changu ambacho kilikuwa kikionesha pia ninatoka nchi gani. Baada ya kugundua ninakotoka akabadili lugha na kuniambia kwa Kiswahili, “habari za Dar es salaam, vipi Buguruni, mambo poa” Wakati naendelea kutafakari hatua ya kufuata, akaanza kuondoka na kuniaga. “Haya bwana, kazi njema!”
Jioni wakati wa mpango wa kazi, nikaitwa na mkuu wangu, nakwambiwa kuwa siku inayofuata, nitaambatana na wake wa Marais na Wakuu wa Nchi ambao watakuwa katika ziara wakiongozwa na mwenyeji wao, Mke wa Rais wa Zambia Maureen Mwanawasa. Siku hiyo ilipofika, tulianza ziara tukiwa katika mabasi mawili, moja likiwa la hao akina Mama Waheshimiwa na jingine la watu waliokuwa kwenye kazi mbali mbali, tukiwemo wanahabari wachache.
Tulipomaliza ziara iliyochukua hadi muda wa mchana, tulirudi katika hoteli ya Pamodzi, ambapo kulikuwa na maonesho ya bidhaa mbali mbali zinazozalishwa na wanawake nchini humo, ikiwa ni pamoija na vito. Mama Maureen hakusita kuwaambia kwa lugha yao akina mama wale, wafanye biashara, kwani hao waliowatembelea ni wake wa Marais. Nilitafsisriwa hicho alichokisema na mwandishi wa gazeti moja la nchini humo.
Baada ya ziara hiyo, akina mama hao wakawa na kikao chao, Mama Maureen Mwanawasa ambaye alikuwa Mwenyekiti wao, alisimama na kuwaambia juu ya ajenda muhimu, iliyohusu azimio lao la kutaka wanawake kupewa nafasi ya madaraka katika kile kinachojulikana kama hamsini kwa hamsini, yaani kama mkakati wa kijinsia wanawake wapewe nafasi katika ngazi mbali mbali katika kiwango cha uwiano sawa na wanaume.
Cha kufurahisha ni kwamba aliwaambia kesho yake watawasilisha hoja, na kwamba kila mmoja aitangulize hoja hiyo kwa mwenzi wake. Na inawezekana kila mmoja aliwasilisha hoja hiyo, maana ilipowasilishwa na Mama Maureen Mwanawasa siku iliyofuata mbele ya Wakuu wa Nchi, hakukuwa na mjadala bali Viongozi hao walipiga makofi kama ishara ya kuiunga mkono, na ikapita, na kuanzia hapo imekuwa ajenda ya kudumu katika Nchi hizo.
Ukiacha hilo, lakini Maureen Mwanawasa amekuwa na ushawishi mkubwa katika mambo mbali mbali enzi ya uhai wake, ikiwa ni pamoja na harakati ya kupambana na umaskini, na pia akiongoza Wake wa Marais na Wakuu wa Nchi katika Jumuiya ya SADC katika kupambana na madhira ya UKIMWI na Virus vya UKIMWI.
Ni Mwanamke ambaye alitumia nguvu ya ushawishi wake katika kupeleka ajenda. Anasifika pia katika kuendesha kampeni za kisiasa kupigania ushindi wa mume wake katika chaguzi.
Maureen alizaliwa April 28. Mwaka 1963 katika eneo la Kabwe nchini Zambia. Aliolewa na Mwanasheria Levy Mwanawasa Mei 07, 1987. Mumewe alifariki mwaka 2008 akiwa madarakani, na Mwenyezi Mungu aliwajalia watoto wanne, ambapo watatu ni wa kike na mmoja ni wa kiume.
Kwa njia ya ushawishi wa akina mama kwenye hamsini kwa hamsini, dada zetu, shemeji zetu, shangazi na mama zetu wanashindwaje kuwashawishi wanaume kushiriki kwenda kanisani? Kwa nini nguvu hii ambayo haihitaji rasilimali fedha, haitumiki kupunguza changamoto hii, ambayo inaelekea kuwa sugu?
Kuna wakati ukihudhuria kanisani, unakuta uwiano ni wanawake kuwa theluthi mbili na wanaume theluthi moja. Unakaa kwenye jumuia unakuta ni wanawake na watoto, labda na mwanume mmoja. Kama akina mama wanaweza kuzengea fedha ya kucha, nywele na marejesho wanashindwaje kuwashawishi wanaume kwende kanisani?