Na Pd. Gaston George Mkude
Amani na Salama!
njili ya leo inatanguliwa na Yesu anapowatuma Mitume wake kumi na wawili, na kuwapa tahadhari juu ya hatari zilizopo mbele yao, na hivyo kuenenda kwa hekima na busara, lakini zaidi sana kudumu katika ujasiri.
Tangu mwanzo, Yesu anawaonesha Wanafunzi wake na hata nasi leo kuwa utume wa kuwa mashahidi wake sio lelemama, na unatutaka kujizatiti. Ni Injili inayotualika kujiandaa kwa gharama ya ufuasi na maisha ya ushahidi.
Mwinjili Matayo anaandika sehemu ya Injili ya leo wakati Wakristo wale wa mwanzo wanapitia madhulumu ya Kaisari Domisiano, aliyetoa amri katika dola zima la Kirumi kuwekwe sanamu yenye sura yake, na kuabudiwa kama mungu.
Hivyo, wale wote waliokataa kuabudu sanamu ile, waliteswa na hata kuuawa kwa amri ya mtawala yule wa Kirumi. Wakristo wale wa mwanzo waliokuwa wenye asili ya Kiyahudi, nao pia walitengwa katika masinagogi kwa kuwa ni wafuasi wa Kristo Mfufuka.
Hivyo ni katika muktadha huo Mwinjili anaandika sehemu ya Injili ya leo kuwafariji, na zaidi kuwakumbusha maneno ya Kristo mwenyewe wakati alipokuwa nao, maana sasa tunazungumzia kizazi cha pili cha Kanisa, na wengi hawakumwona Yesu uso kwa uso, zaidi ya kupokea Habari Njema kutoka kwa Mitume wake.
Ni Kanisa teswa lililokuwa likiishi imani yake kwa hofu na kujificha, huku wakigubikwa na hofu kubwa kutoka maadui wao wakubwa wawili, ambao ni Dola la utawala wa Kirumi na Wakuu wa Masinagogi, au Wakuu wa Dini ya Kiyahudi.
Mwinjili anawakumbusha Wakristo wale wa kwanza kuwa tayari Bwana na Mwalimu wao alishawatabiria juu ya magumu, mateso na madhulumu. Hivyo sio kitu kigeni, na hawapaswi kukata tamaa wala kurudi nyuma katika safari yao ya ufuasi na kuwa mashahidi wa Habari Njema ya ukombozi. Tunaona pia Mtume Paulo anapomwandikia waraka ule wa pili Timoteo akisema;
“Kila mtu anayetaka kuishi maisha ya kumcha Mungu katika kuungana na Kristo Yesu, lazima adhulumiwe.” (2Timoteo, 3:12). Mtume Paulo anaandika naye kipindi kile kile cha madhulumu na mateso ya Kanisa lile la mwanzo.
Ni katika mazingira hayo ya mateso na madhulumu tunapoona Yesu anawaalika Wanafunzi wake kutoogopa, kutokukubali kurudi nyuma kwa sababu ya uoga na hofu. Tunasikia Yesu akiwaalika mara tatu “msiogope”. Uoga unaweza kuwa na upande chanya kututahadharisha na hatari inayokuwa mbele yetu, na hivyo kuenenda kwa tahadhari, lakini ina upande hasi, hasa pale tunapoacha kutawaliwa na uoga na hofu.
Kila tunaporuhusu uoga ututawale hapa, tunakosa uhai na maisha, tunakosa pumzi na uwezo wa kuishi au wa kusonga mbele katika wito na utume wetu. Kuruhusu uoga utawale maisha yetu, ni kukubali kushindwa kusonga mbele, ni kukubali kujimaliza na kujiangamiza sisi wenyewe.
Uoga ni adui mkubwa katika maisha yetu ya ufuasi. Tunakuwa waoga kupoteza nafasi zetu za heshima kwa kuwa tu wafuasi wa Yesu Kristo, kupoteza marafiki zetu, kupoteza mali na utajiri wa dunia hii, kudharauliwa na wengine, na mara nyingine hata kupoteza maisha yetu. Kila anayeruhusu kutawaliwa na uoga, huyo anapoteza uhuru wa kweli. Anakuwa sawa na mmoja mwenye ugonjwa wa kiharusi kwa kukubali kutawaliwa na uoga.
Na ndiyo maana Yesu anarudia mara tatu nzima ili kututahadharidha na hatari ya uoga katika maisha ya ufuasi.
Wakati wa sherehe za Jubileo Kuu ya Mwaka 2000, Mtakatifu Papa Yohane Paulo II (1978-2005) anatuambia; Miaka elfu mbili ya Ukristo duniani inatambulishwa kwa damu ya mashahidi wa nyakati mbali mbali.
Ndiyo maana anaendelea kutuonesha kuwa Kanisa limekuwa na mashahidi wengi, au wafiadini wengi katika karne ya 20 kuliko hata wale wa Kanisa la mwanzo.
Na hata leo katika nyakati zetu bado tunashuhudia jinsi Kanisa na Wakristo wanavyopitia madhulumu mengi mahali pengi duniani. Ni zaidi ya madhulumu ya Wafalme wale katili wa Kirumi, yaani Nero, Domisiano, na hata Deoklasiano kwa pamoja!
Anayepelekwa kutangaza Habari Njema anaweza kutawaliwa na uoga wa kushindwa katika misheni yake. Na ndiyo maana Yesu anatukumbusha kuwa hata kama tutakutana na magumu, daima Injili yake itaenea na kusambaa ulimwenguni kote.
Magumu, mateso, kukataliwa na madhulumu, ni sehemu muhimu ya maisha ya ushuhuda wa imani yetu. Ni Yesu anatangulia kutuambia hata nasi leo kuwa njia ya maisha ya ushahidi, ni hiyo ya magumu na mateso.
Yesu kwa kutuhakikishia hilo, anafanya marejeleo kwa Marabi wa nyakati zake ambao walibaki na wanafunzi wao na kuwafundisha sirini mpaka pale mmoja alipohitimu ndipo aliruhusiwa kwenda kufundisha katika viwanja na masinagogi.
Ndiyo kusema kwamba Yesu anatusisitizia hata pale tunapoona kazi yetu haina mafanikio makubwa kwa macho, na mitazamo yetu ya kibinadamu hakika bado litazaa matunda ni kama vile mbegu iliyozikwa ardhini.
Mfano wa wazi ni watesi wa Yesu mwenyewe mara baada ya kumuua na kumzika na kuweka jiwe kubwa katika mlango wa kaburi, walijiridhisha na kujihakikishia kuwa sasa wameshinda na kufaulu kumnyamazisha mtu yule kutoka Galilaya. Siku ya tatu akafufuka na kuwa mzima tena! Amefufuka kama mbegu iliyokuwa imezikwa ardhini, na sasa imechipua na kuleta matumaini na mwanga mpya.
Sababu ya pili inayoweza kutuletea uoga na hofu, ni madhulumu na mateso, na hata kifo. Na ndipo Yesu pia anatuhakikishia kuwa hakuna ushindi wowote unaoweza kupatikana kwa wale wanaotesa mwili, kwani kila anayekuwa tayari na jasiri kumfuasa Yesu na kuwa shahidi wa Injili, huyo anajaliwa uzima wa milele, maisha ya kweli sasa, na hata milele.
Kila mfuasi wa kweli huyo anapokea siyo tu maisha ya kibailojia, bali maisha ya muunganiko na Mungu mwenyewe. Hivyo ni maisha ya hapa duniani na milele yote. Mtume Paulo anapowaandikia Warumi anawakumbusha pia ukweli huo; “Ni nani awezaye kututenga na upendo wa Kristo? Je, ni taabu, au dhiki, au mateso, au njaa, au ukosefu wa nguo, au hatari, au kifo? (Warumi, 8:35-39).
Lakini anaendelea Yesu na kututahadharisha kumwogopa mmoja anayeangamiza, si mwili tu, bali pamoja na roho.
Kwa kweli tafsiri sahihi siyo kitu kinachokuwa nje yetu, bali kila mmoja wetu anacho ndani mwake tangu kuzaliwa kwetu, yaani ndiyo nguvu ile ya mwovu inayotuambia kila mara kuenenda kinyume na njia na mipango yake Yesu Kristo.
Kila wazo linalopinga mpango mzima wa Yesu, huwa linapelekea katika angamio langu na lako kwani tunaangamia, si tu mwili, bali pamoja na roho. Kila mmoja wetu anajua ni nini katika maisha yake kinamkinza katika kuiishi na kuwa shahidi wa Injili, na tukichunguza tunaona jambo au kitu hicho asili yake ni ndani mwetu sisi wenyewe. Ule uasi na uovu tunaokuwa nao ndani mwetu unaotushawishi kuenenda kinyume na mapenzi na maagizo ya Mungu, na Neno lake.
Sababu ya tatu inayotuepelekea kuogopa sasa inagusa si tu sisi, bali hata na wale wanaokuwa karibu nasi. Na ni hapo Yesu anapotuhahakishia ulinzi wa Mungu Baba, kwani sote tu wa thamani kubwa mbele yake.
Anatumia mifano ya shomoro na nywele. Shomoro kwa nyakati za Yesu walihesabiwa kuwa ni viumbe wasio na thamani, kwani walikuwa ni ndege waharibifu kwa mazao, na hasa ngano ikiwa bado shambani. Hivyo Wayahudi walipowabariki viumbe vyote vya Mungu, hawakuwabariki shomboro, kwani ni waharibifu, ila leo Yesu anatuonesha kuwa mbele ya Mungu, kila kiumbe kina thamani kubwa.
Hivyo kutuhakikishia kuwa hatuna sababu ya kuwa na uoga wala hofu, hata kama mbele yetu kuna mateso na madhulumu makubwa. Mungu anajua hata hesabu ya unywele mmoja, vile sisi hatuwezi kuhesabu nywele, lakini mbele ya Mungu, sisi sote kama viumbe vyake, tuna thamani kubwa.
Yesu anamalizia kwa ahadi kuwa kila anayemkiri mbele ya watu, huyo atamkiri mbele za Baba yake wa Mbinguni. Ni hakika kuwa tunatambuliwa na Mungu, hata sisi tukiwa kweli wafuasi wa kweli wa Kristo bila kujali hatari zinazoweza kutukabili na hata kutuzuia kuwa mashahidi.
Daima mfuasi hana budi kumtegemea Mungu katika kila hali za maisha ya ufuasi, kwani neema yake ni ya kutosha.
Tafakari njema na Dominika Takatifu!