KIGOMA
Na Mathayo Kijazi
Katika kuhakikisha familia, jamii, na hata Kanisa kwa ujumla linaendelea kuwa na watu wenye maadili ya kumpendeza Mungu, ni lazima familia zijengwe vyema, ili ziweze kudumu katika misingi iliyo bora.
Zipo njia mbalimbali zinazoweza kutumika kujenga jamii iliyo bora kupitia katika familia zao, zikiwemo semina za Kanisa, mikutano, makongamano, pamoja na mafundisho mbalimbali.
Katika jitihada hizo za kujenga familia, Utume wa Uimarishaji wa Familia Tanzania (UFATA), hivi karibuni ulifanya Mkutano wake Mkuu wa Kitaifa katika Jimbo Katoliki la Kigoma.
Vile vile, ndani ya Mkutano huo ilifanyika Semina iliyohusisha mada mbalimbali zilizolenga familia, mwenendo wake, pamoja na tafakari mbalimbali.
Akiwasilisha mada isemayo ‘Familia imara ni msingi wa utu wa mtu’, Mkuu wa Chuo cha Songea Catholic Institute of Technical Education, kilichopo Songea, mkoani Ruvuma, Padri Longino Rutangwelera Kamuhabwa wa Jimbo Katoliki la Bukoba, anasema kwamba kwa kuumbwa kwake na kwa hulka yake, utu wa mtu ni wa kuheshimiwa na umetakaswa.
Padri Kamuhabwa anasema kwamba Familia ni Taasisi ya Kimungu kati ya wanadamu, kwa ajli ya kuendeleza na kulinda heshima ya utu wa mtu, na kwamba kuheshimu familia na utu wa mtu, ni kumheshimu Mungu aliye chimbuko lake.
Anaongeza kwamba mwanadamu anatakiwa kuheshimiwa na kuthaminiwa kama njia mojawapo ya kumheshimu na kumthamini Mungu, kwani ameumbwa kwa malengo ya kumjua, kumpenda, kumtumikia Mungu na kutafuta Ufalme wake.
Padri huyo anabainisha pia kuwa mwanadamu ni wajibu wake kutambua kwamba ameumbwa pamoja na wanadamu wengine, kwani huo ni mpango wa Mungu kuwa mwanadamu atimize malengo ya kuumbwa kwake akiwa kundini.
Anasema pia kwamba mwanadamu ni muhitaji, mhanga na dhaifu, hivyo, anahitaji kuhubiriwa, kulindwa, kutetewa, kukemewa pamoja na kuelekezwa.
Anabainisha pia kwamba katika kuwa kiumbe muhitaji, mwanadamu kwa hulka yake, Mungu alimuumba mtu akiwa na njaa na kiu ya kufikia ukamilifu, na kuongeza kuwa ni katika hali hiyo, mtu hutafuta, husali, hufanya kazi ili afikie kile cha kumfanya awe mkamilifu. Katika kutafuta huko, Padri huyo anasema kwamba mwanadamu pengine hupatia, na pengine hukosea.
Pia, Padri huyo anasema kwamba nyenzo za kumsaidia wanadamu kufikia kile anachokihitaji, ni pamoja na Sala, Neno la Mungu, Maisha ya sakramenti, pamoja na Maisha ya familia.
Vile vile, anasema kuwa kwa hulka yake, mwanadamu ameumbiwa kwanye jamii (familia), na kwa asili yake, ana mwelekeo wa kuishi au kushirikiana na wanadamu wengine.
“Mwanadamu anafaidika kwa kushirikiana na wanadamu wengine. Kukamilisha na kukamilishwa na wengine (complementarity principle). Kutegemeza na kutegemezwa na wengine (synergy principle). Mtu ni ufunuo na uwepo wa Mungu kati ya watu (transcendental being)…
“Kadiri ya Edith Stein (Mtakatifu Theresa wa Msalaba) mtu ni Epiphania - anafunua wema na upendo wa Kimungu kwa wengine. Kadri ya Mtakatifu Thomas Aquinas, kupitia ubinadamu wetu, Mungu yu pamoja nasi = Emmanuel. Kristu aliutwaa ubinadamu wetu ili sisi tukwezwe na kuushiriki Umungu wake. Kwa hiyo, mtu ni ufunuo wa uwepo wa Mungu kati yetu. Mtu ni zaidi ya yale unayoyaona,” anasema Padri huyo.
Sambamba na hayo, Padri Kamuhabwa anaongeza kwamba mwanadamu ni kiumbe hisia, kwani kwa hulka yake anaweza kufurahi au kukasirika; kupenda au kuchukia; kuwa na vionjo mbalimbali; kukubaliana pamoja na kutofautiana na wengine.
Anasema kwamba hiyo inaleta uhalali wa mtu kupenda na kupendwa, kujali na kujaliwa, kuheshimu mawazo na maoni ya mtu, kumpa mtu nafasi ya kuchagua anachokitaka, na kuacha asichokipenda.
Kwa nini utu wa mtu uheshimiwe na kulindwa?
Padri Kamuhabwa anabainisha kwamba ni vizuri kutumia sababu moja kati ya hizi, ili kujenga hoja ya kulinda heshima na utu wa mtu; Mtu ni sura na mfano wa Mungu (Mwa, 1:26); Mtu kajaliwa akili na utashi wa kumtafuta Mungu (Isaiah, 1:17-19); Mungu kapitia kwa mtu kajifunua kwa viumbe wote (In, 14:8-9); pamoja na; Mungu kamchagua mtu na kuweka agano naye (Mwa, 9:13; Kut. 19:5).
Sambamba na hayo, anasema kwamba familia ni taasisi ya kuenzi na kuheshimu utu wa mtu, kwani hiyo ni taasisi ya wanadamu aliyoianzisha Mungu ili kupitia kwenye taasisi hiyo, watu washirikishane upendo wa Kimungu, na watu washiriki kazi ya Mungu ya uumbaji.
Pia, anabainisha kwamba taasisi hiyo ni ya wanadamu kwa sababu inaundwa na wanadamu (nuclear and extended). Na pia ni ya Kimungu kwa sababu mwasisi, mtegemezaji na malengo yake ni Mungu.
Vile vile, anasema pia kwamba taasisi hiyo ni ya upendo, kwa sababu kiungo chake ni upendo, ni ya uumbaji kwa sababu inaendeleza umbaji.
Njia za kuenzi na kuimarisha familia:
Akitaja njia zinazoweza kutumika ili kuimarisha familia, Padri huyo anabainisha kwamba ni lazima kuwepo na sala, kuiombea na kusali pamoja; ijikite katika kusoma na kuishi Neno la Mungu; Maisha ya Sakramenti; ipate neema za Sakrameti; malezi endelevu; ianze na Mungu na ibaki na Mungu; Maadhimisho endelevu; kushika amri ya mapendo, kufanya kumbukizi za matukio muhimu ya kifamilia, pamoja na kuhuisha mahusiano.
Matishio dhidi ya familia:
Akitaja mambo yasiyofaa na yanayoonekana kuwa tishio katika familia, Padri Kamuhabwa anasema kwamba mambo hayo ni pamoja na familia kuanzishwa kiholela.
Anaongeza kuwa kadri ya mpango wa Mungu, familia huanza kupitia ndoa halali, tofauti na hilo, ni mwanzo potofu, matokeo yake ni matokeo na mwisho potovu.
Vile vile, anasema kwamba upotoshwaji wa sifa za wanafamilia ni moja ya tishio, kwani familia huundwa na baba, mama na watoto. Upotovu katika jinsia za wazazi ni tishio la familia.
SOMA ZAIDI....