Na Mwandishi wetu
Mfuko wa Self (Self-Microfinance Fund) unaomilikiwa na Serikali chini ya Wizara ya Fedha na Mipango, umefanikiwa kuikuza Sekta Ndogo ya Fedha na Wajasirimali kwa kutoa mikopo yenye thamaini ya Shilingi bilioni 324 katika kipidi cha kufikia Desemba 31 mwaka 2023.
Aidha, Self imejipanga kuhakikisha inasogeza zaidi huduma zake kwa kuongeza matawi nchi nzima kutoka 12 ya sasa hadi kufikia 20 ifikapo mwaka 2026, kwa kutengeneza mifumo mizuri ya ufuatiliaji na usimamizi wa fedha ili kuwafikia watu wengi, wakiwemo wakulima katika maeneo ya vijijini.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Self, Mudith Cheyo alisema hayo hivi karibuni katika Mkutano wake na Wahariri na Waandishi wa Vyombo yya Habari nchini, akielezea mafanikio, mipango mikakati na changamoto katika Taasisi hiyo ya fedha.
“Sisi kama Self, tangu tulipokabidhiwa mamlaka hii mwaka 2015 kuiinua sekta ndogo ya fedha, tumeweza kufanya kazi kubwa katika utoaji wa mikopo kwa wajasiriamali na Taasisi 200 nchi nzima …na katika hilo tumesaidia sana katika kuikuza na kuiendeeleza Sekta Ndogo ya Fedha nchini,” alisema Cheyo.
Cheyo alisema kuwa pamoja na mambo mengine, kwa sasa Self inaendelea na mikakati yake ya kujiimarisha zaidi, kwani tangu ilipopewa mtaji na serikali ili kuikuza na kiendeleza Sekta Ndogo ya Fedha kwa njia ya mikopo, wameiwezesha taasisi hiyo kujitegemea, na haijawahi kurudi serikalini kuomba tena mtaji.
Cheyo alifafanua kwamba Serikali iliwapatia mtaji wa Shilingi bilioni 56, na kwa usimamizi mzuri wa Taasisi hiyo, wameweza kutengeneza faida na sasa wamefikisha Shilingi bilioni 62, na imekuwa ikitoa gawio la Shilingi milioni 240 hadi milioni 250 kwa Serikali.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Biashara na Masoko wa Mfuko wa Self, Petro Mataba, alibainisha kuwa katika kutekeleza majukumu yake, Self ilitoa elimu ya fedha kwa wajasiriamali 1517, kuhusu namna ya kusimamia fedha na uendeshaji biashara.
Akizungumzia changamoto zinazoikabili Self, Mataba alisema kuwa wakopaji wengi wamekuwa wakishindwa kurejesha mikopo yao, lakini uongozi wa Taasisi hiyo umejipanga na kufanikisha kudhibiti mikopo chechefu kwa asilimia 10.
Aidha, alisema kuwa changamoto nyingine ni wakopaji kushindwa kutekeleza mipango waliyojiwekea, na hivyo kuelekeza fedha za mikopo katika mambo ambayo hawajakusudia, matokeo yake wanakwama kulipa madeni yao.
Kwa upande wa mipango ya baadaye ya Taasisi hiyo, Mataba alisema kuwa mfuko huo umejipanga kupanua wigo wake kwa kuwafikia watu wengine hadi maeneo ya vijijini, ili kuwawezesha watu wengi katika sekta ndogo ya fedha kupata mikopo ili kujikwamua kiuchumi.
Mpango mwingine ni kuongeza ufanisi kwa kutumia njia ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ili kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi, na kutoa huduma endelevu kwa watu.