DAR ES SALAAM
Na Mwandishi wetu
Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya limepata Askofu mpya Msaidizi Mhashamu Askofu Mteule Godfrey Jackson Mwasekaga.
Baba Mtakatifu Fransisko alifanya uteuzi huo hivi karibuni ambapo kabla ya uteuzi huo, Askofu Msaidizi Mteule Godfrey Jackson Mwasekaga, alikuwa Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Fransisko wa Assisi, Mwanjelwa, Jimboni Mbeya, na pia alikuwa Makamu Askofu wa jimbo hilo.
Alisoma katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Augustino, Peramiho, Jimbo kuu Katoliki la Songea, na hatimaye akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 14 Julai, 2005 kwa ajili ya Jimbo kuu la Mbeya. Hadi kuteuliwa kwake alikuwa ni Makamu Askofu Jimbo Kuu la Mbeya, Mkurugenzi wa Idara ya Katekesi Jimbo, na Mkurugenzi wa Kituo cha Katekesi na Paroko wa Mwanjelwa.
Askofu Msaidizi Mteule Godfrey Jackson Mwasekaga (pichani) alizaliwa Machi 17 mwaka 1976 huko Kyela, Mbeya. Alisoma katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Augustino, Peramiho, Jimbo Kuu Katoliki la Songea, na hatimaye alipewa Daraja Takatifu ya Upadri Julai 14 mwaka 2005 kwa ajili ya Jimbo Kuu la Mbeya.
Tangu wakati huo kama Padri, aliteuliwa kuwa Paroko-usu Parokia ya Mtakatifu Claver, Mlowo, kati ya Mwaka 2005 hadi Mwaka 2008. Mkurugenzi wa Idara ya Katekesi Jimbo, na Mkurugenzi wa Kituo cha Katekesi kati ya Mwaka 2006 hadi mwaka 2008.
Alitumwa na Jimbo Kuu la Mbeya kujiendeleza kwa masomo katika Taalimungu katika Taasisi ya “Salesiano San Tommaso Messina” nchini Italia.
Baadaye akazama zaidi katika Taalimungu na kujipatia Shahada ya Uzamivu katika Taalimungu kutoka katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Wasalesian, kilichoko Roma, kati ya Mwaka 2008 hadi mwaka 2017.
Baada ya masomo yake, alirejea Jimboni Mbeya na kuteuliwa kuwa Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Petro Claver, Mlowo, kati ya Mwaka 2018-2019.
Kuanzia mwaka 2017 ni Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Katekesi Jimbo Kuu la Mbeya, Mkurugenzi wa Kituo cha Katekesi na Mratibu wa Liturujia ya Kanisa. Na pia kuanzia mwaka 2019, akateuliwa kuwa Makamu Askofu Jimbo Kuu la Mbeya, na Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Fransisko wa Assisi, Mwanjelwa, Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya.