DAR ES SALAAM
Na Mathayo Kijazi
Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Yohane wa Mungu – Vituka, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Patrick Bwakila amewataka watoto kutokuufananisha mkate uletao uzima (yaani Mwili wa Kristu) na mikate mingine, kwani wanapokula Mkate huo, wanamla Kristu mwenyewe.
Aliyasema hayo wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika, iliyokwenda sanjari na kuwapatia watoto hao Sakramenti ya Ekaristi Takatifu katika Parokia ya Yohane wa Mungu – Yombo Vituka, jimboni humo.
“Ndugu zangu wanangu wapendwa, Mama Kanisa alitufundisha kwamba Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristu, Mungu kweli na Mtu katika maumbo ya mkate na divai…
“Kumbe, mkate tunaokula leo, siyo ule wa mama mpika chapati, hapana, ni Kristu mwenyewe ndiye mnayemla leo. Na Kristu mwenyewe anatuambia, aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu, huyo hukaa ndani yangu, na mimi hukaa ndani yake. Huu ni mkate wa uzima, mkate uletao uponyaji, afya ya roho, mkate unaotustahilisha sisi huurithi na kupata uzima wa milele,” alisema Padri Bwakila.
Padri Bwakila aliwaonya watoto hao kuepuka kumuasi Kristu mara baada ya kupokea Sakramenti hiyo Takatifu, na kuongeza kwamba atakayefanya hivyo, atatakiwa kuacha kushiriki sakramenti, kwani amemkana na kumkimbia Kristu.
Pia, aliwataka kukumbuka kwamba kwa Sakramenti hiyo ya Ekaristi Takatifu waliyoshiriki katika adhimisho hilo la Misa Takatifu, wametengeneza mahusiano ya kudumu na Yesu Kristu, ambaye ndiye waliyemla.
Mmisionari huyo wa Shirika la Watumishi wa Wagonjwa(Wakamiliani), aliwasihi watoto hao kujitahidi kujibidiisha siku zote, ili watamani na waendelee kupokea chakula hicho ambacho ni kitakatifu.
Aliongeza kwamba haipendezi kwa mtoto ambaye amepokea Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, na baada ya hapo, haonekani kanisani kushiriki katika Adhimisho la Misa Takatifu.
“Leo umepokea Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, baada ya hapo unasema sasa Kanisa ‘bye bye’. Ukifanya hivyo, na Yesu naye atakwambia ‘bye bye’. Utatoroka kanisani, utaliacha kanisa, utaenda kuhangaika, baadaye likikupata tatizo, utaanza kusema ‘Mungu wangu mbona umeniacha,” alisema Padri huyo.
Aliwasisitiza kutokumwacha Mungu ambaye tayari wameshatengeza mahusiano mazuri naye, kwani faida ya kuwa karibu na Mungu wataiona mbinguni.