DAR ES SALAAM
Na Dkt. Felician Kilahama
Ni vema na haki kumshukuru Mungu Mwenyezi kwa kutuwezesha kuendelea kuishi, tukipumua bila ya athari zozote. Hayo ni mapenzi yake, siyo kwa ridhaa au nguvu zetu wenyewe, bali ni kwa rehema zake kuu, hivyo, jina lake lihimidiwe.
Katika sehemu ya kwanza, Makala iliishia kwenye kipengele kilichozungumzia kuhusu vijana kupenda kupata fedha kirahisi, mfano, kupitia masuala ya ‘kubeti’.
Hatinaye, kueleza ‘ipo michezo mingine mingi inayochezwa kupitia mitandao na vyombo mbalimbali vinavyohimiza Watanzania kucheza ili kujipatia fedha kirahisi.’ Haya yote yanafanyika kwa mwelekeo wa kamari (gambling au gaming), na vijana wengi wamevutwa.
Kimsingi, masuala yanayohusiana na kucheza kamari siyo mazuri, maana yanapelekea mhusika kupotoka na kujikuta akitenda maovu. Kwanza, kuna kutekwa kifikra/kiakili na kupoteza maarifa ya kufanya uamuzi sahihi.
Kila wakati mhusika anabaki akijiweka kwenye nafasi ya kushinda, huku akitumia fedha ambazo harudishiwi iwapo hatashinda. Pili, michezo ya aina hiyo inajenga lango la kutenda uovu, ikiwemo wizi na, au udanganyifu.
Mhusika iwapo hana fedha za kumfanya acheze, atafanya kila linalowezekana apate fedha kihalali au vinginevyo, ili mradi afanikishe lengo.
Kihalali anaweza akauza vitu vyake, mfano, nguo, viatu, simu kiganjani au akahangaika akapata kibarua na kupata fedha akacheze kwa mtazamo kuwa atashinda na kupata fedha atajirike.
Vinginevyo, kuna uwezekano mkubwa wa kujenga tabia ya kudokoa mali za wengine, au kuiba fedha na vitu vingine nyumbani, mitaani na hata kupora, ili mradi afanikishe lengo lake.
Kwa bahati mbaya, mtazamo huu usiofaa kwa vijana ambao ndiyo nguvukazi kubwa ya taifa letu, unachochewa na baadhi ya matangazo yanayofanyika kupitia vyombo mbalimbali vya matangazo.
Mathalani, luninga, redio, magazeti na hata simu janja au za kawaida, kwamba kuna wakati ninapofungua sehemu ya ujumbe kwenye simu; mara kwa mara huwa nakuta ujumbe kutoka namba fulani wakitangaza, ‘wewe umekaribia kushinda kiasi fulani cha fedha, mathalani, milioni mbili, tuma neno fulani ushinde.’
Kadhalika, unaambiwa ‘weka Tshs 500 ujipatie hadi Tshs milioni tatu na bonasi ya Tshs 200,000 papo hapo,’ au ‘wewe ni milionea mpya, chagua namba 1 hadi 6 uweze kushinda hadi milioni mbili na ‘Jackpot’ ya Tshs 300,000 kila siku.’ Vile vile maneno “funua pesa mkwanja tele maisha mapya …”
Wakati mwingine unakuta kwenye gazeti, kumewekwa, mathalani, “Supa Jackpot” (TZS 1,150,172,000 kwa TZS 1,000 tu). Kijana akiangalia tarakimu hizo na kwa lugha ya mitaani: kwa buku tu, anahamasika kucheza. Lakini ili aweze kushinda na kupata hizo fedha, atacheza mara ngapi? Yote haya ni katika kukengeuza akili za wengi na hasa vijana ambao ndiyo kundi kubwa linaloathirika zaidi.
Wakati mwingine yanaletwa maswali kadha wa kadha, na mengi ni ya kimichezo, hasa soka na, au kuigiza. Pia, nyimbo hasa ‘bongo fleva’ na waimbaji wake. Nia ni watu wengi wajibu ili wakwapue hela kutoka kwenye bando kupitia mitandao husika. Katika uhalisia wa michezo kama hiyo, wengi wanaangamia, na wataangamia kwa kukosa maarifa.
Kimsingi, michezo (gaming/gambling) ni aina ya kamari hata kama tukisema imeboreshwa, lakini ni pata potea. Inafanya wengi wapoteze fedha zao kwa matumaini ya kupata/kushinda, wakati wanaoshinda ni wachache sana kulingana na idadi ya wanaocheza.
Kabla mhusika hajacheza mchezo wowote wa kubahatisha, ni lazima kujua asilimia ya kushinda, au uwezekano wa kushinda (probability rating); na hilo ni jambo la msingi, mathalani, kuna wachezaji milioni moja kwa mchezo mmoja, na pengine anatakiwa apatikane mshindi mmoja, washindi kumi, au washindi mia moja. Kinachotakiwa kukifahamu ni kujua kwa kiasi gani unaweza kushinda.
Kwa kundi la kwanza zitatolewa milioni moja; kundi la pili milioni kumi (washindi 10) na kundi la tatu milioni miamoja (washindi 100). Kiwango cha ushindi ni asilimia 0.0001; 001 na 0.01 kwa makundi hayo matatu mtawalia. Hali hiyo inaonyesha kuwa ni asilimia ndogo sana ya mhusika kuweza kuibuka mshindi, ndiyo maana ikaitwa ‘bahati nasibu’.
Kadhalika, baadhi ya vijana hutembeza barabarani baadhi ya bidhaa mbalimbali mikononi wakitafuta wateja.
Wengine wanatumia muda mrefu kutoka eneo moja kwenda jingine wakitafuta wanunuzi.
Jioni inapoingia, mhusika anapoona hana kitu mfukoni na njaa inamuuma, analazimika auze kwa bei mnunuzi anayotaka, ili mradi apate kiasi cha kumsaidia aweze kujikimu. Baadhi wana familia hivyo hujikuta katika changamoto hatarishi kiasi cha kulazimika kutenda uovu kwa kigezo cha hakuna jinsi, bora nusu shari, kuliko shari kamili, anaitelekeza familia yake.
Tujiulize kwa mustabali wa taifa letu, je, vijana kutaka kupata fedha haraka haraka kupitia michezo mbalimbali ya kifedha kama ‘kubeti’ na mingineyo, kitaifa ni jambo jema? Je, vijana na watu wengine tunatumia muda vizuri kwa manufaa yetu, familia na taifa kwa ujumla?
Kimsingi, matumizi halisi ya ‘muda’ kwa nyakati hizi ni suala la kuwekewa mkazo. Kila siku tunapoamka tunafanya nini? Maana unakuta makundi ya watu wa rika mbalimbali wakiongelea masuala ya michezo, mfano, kusajili wachezaji, hususani timu za Tanzania na za Uingereza.
Kadhalika, unaona vijana wanatumia muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii ‘wakichati’ kupitia simu za kiganjani. Je, ni matumizi halisi ya muda? Siku ina saa 24 na wiki ina siku saba au saa 168.
Kawaida binadamu anatakiwa kulala usingizi (angalau saa 8 kwa siku), kwa wiki atatumia saa 56 kitandani. Kwa wiki, ukiondoa siku moja ya kuabudu/kusali, kuna siku sita za kufanya kazi. Hii inamaanisha kuwa tukiondoa saa za kusinzia, kwa siku tuna saa 16 za kufanya kazi, na ndani ya siku sita, ni takribani saa 96 za kufanya kazi.
Muda huu ukitumiwa kwa kiwango cha kufikia asilimia 75 (takriban saa 12 kwa siku, sawa na saa 72 kwa wiki), ukatumika kuzalisha mali na huduma ili kujipatia kipato, hakika tutajikwamua kimaendeleo (muda uliobaki, takriban saa 4 kwa siku au saa 24 kwa siku sita za kazi; ukatumika kwenda na kutoka mahali pa kazi, pengine kupata mapumziko mafupi wakati mhusika akiwa kazini).
Uzoefu unaonyesha kuwa wengi wetu, wakiwemo vijana, hatuzingatii matumizi mazuri ya muda, iwe ofisini, viwandani au kwingineko, kwani bado kuna kusuasua bila maelezo toshelezi. Hivyo, vijana tujiepushe kufuata mkumbo kwa masuala yasiyotuletea maendeleo ya kweli kimaisha.
Serikali iweke Sera thabiti kuinua maisha ya Watanzania hususan vijana. Tuliporuhusu matumizi ya ‘bodaboda’ na ‘bajaji’ kutoa huduma za usafiri na usafirishaji, jambo hilo limekuwa faraja kwa vijana wengi kujiajiri au kuajiriwa. Wanaoitumia fursa hiyo kwa umakini baada ya miaka miwili au mitatu, wanasonga mbele ipasavyo.
Mkakati wa Serikali wa kuinua zaidi shughuli za kilimo kwa lengo la kuwapatia vijana ajira na kuimarisha au kuendeleza uchumi wa taifa, upewe msukumo zaidi ili kuhusisha sekta mbalimbali za umma na binafsi. Kupanuliwe wigo ili vijana wengi waweze kujipanga vizuri kulingana na uwezo waliopewa na Mwenyezi Mungu.
Wenye ari ya kufuga wafanye hivyo kitaaluma na kibiashara; wenye kumudu masuala ya uvuvi, misitu na nyuki na utalii, pamoja na biashara, wafanye hivyo bila shida. Shughuli za ugani ziimarishwe ili kuhakikisha mafanikio tarajiwa yanapatikana.
Tukiongeza tija kwa bidhaa nyingi kuzalishwa hapa nchini, tutajenga uwezo wetu wa kujitegemea. Wakati huo huo, tutasaidia idadi kubwa ya vijana kuachana na ‘michezo potofu’, hivyo kuimarisha ‘nguvukazi’ ya taifa letu kwa faida ya wengi.
Halmashauri zote nchini na Mamlaka za Mikoa na Wilaya, zihakikishe kuna mazingira mazuri ya kuwezesha vijana kutumia rasilimali ardhi kwa faida na weledi mkubwa, mathalani, Halmashauri zianzishe mifumo thabiti ya kuunganisha ‘nguvukazi-vijana’ kwenye maeneo yao.
Kuweka fursa za ‘mitaji’ kuwakopesha vijana; tukizingatia masharti nafuu na kuweka ‘kanzidata’ kuhusu vijana kuhusiana na taaluma au uwezo wao.
Katika kuyatekeleza hayo, uwazi na uadilifu vizingatiwe ipasavyo. Vijana wajengewe mazingira ya kuwa waaminifu katika kutumia muda vizuri na kutimiza wajibu wao ipasavyo. Viongozi na wenye madaraka kwa ngazi zote, tuwe waadilifu, siyo kwa maneno tu, bali kimatendo.
Tuchukie ‘udanganyifu, wizi, kutoa au kupokea rushwa, au kukwapua’ mali za umma. Hayo yawe mwiko mkubwa katika sifa za kiongozi mzuri anayetumainiwa na wengi.
Tamaa za kujitajirisha ‘chapuchapu’ (yaani haraka haraka) kwa kutumia njia haramu na zisizofaa, vikomeshwe, na watakobainika wachukuliwe hatua kali za kiutawala na kisheria. Tafakari kwa kina, chukua hatua madhubuti.