Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Uinjilishaji katika Nchi za Burundi na Kongo Brazaville

Misioni ya Rumonge, nchini Burundi. Misioni ya Rumonge, nchini Burundi.

HISTORIA YA KANISA

Katika safu hii ya Chimba Chimba Historia ya Kanisa wiki iliyopita tuliwaletea mada ya historia ya uinjilishaji katika nchi ya Rwanda. Leo tunaendelea kuwaletea historia ya uinjilishaji nchini Burundi na Kongo Brazaville. Sasa endelea…

Wamisionari wa kwanza, Wamisionari wa Afrika, walifika Burundi kutokea Ujiji, Tanzania, mwaka 1879 wakingozwa na Padre Deniaud, na kufungua misioni Rumonge. Lakini mwaka 1881 kwa chuki ya Waarabu wakishirikiana na baadhi ay Waafrika, walimwua Padri na wenzake wawili. Hapo ikabidi misioni isitishwe. Sehemu ya Burundi walibaki Kibanga ukingoni mwa Ziwa Tanganyika.
Mwaka 1895 Burundi iliunganishwa na Vikariati ya Unyanyembe, Tanganyika.  Parokia za kwanza zilifunguliwa ni Muyinga mwaka 1898 na Mugera mwaka 1899. Historia ya mwanzo ya Burundi ilienda sambamba na historia ya Rwanda.
Mwaka (1912-1922), ziliunganisjwa katika Vikariati moja ya Ruvu, chini ya Askofu Hirth. Jamii ya Burundi ilikuwa na mshikamano mkubwa kuliko ule wa Rwanda. Vile vile kati ya watawala, licha ya Watutsi yalikuwepo makabila mengine mawili, Bahima ambao ni ukoo mmojawapo wa Watutsi, na Ganwa ambao ni Wahutu, lakini wa damu ya kifalme. Hii ilileta kidogo changamoto kati ya Watutsi.
Vile vile, kuna familia nyingi zaidi zenye damu mchanganyiko wa Kitutsi na Kihutu. Dini ilienea haraka zaidi Burundi kuliko Rwanda, baada ya Vita Kuu ya Pili (1939-1945) palikuwepo Wakatoliki 600,000 ambao walikuwa mara mbili ya wale wa Rwanda, na miaka kumi baadaye kabla ya Uhuru mwaka 1959 walishafikia Wakatoliki 1,200,000 ambao walikuwa asilimia 55 ya wakazi wote.
Miito ya Upadre ilikuwa michache, walipata Padre wa kwanza Mwafrika mwaka 1925 na Askofu wa kwanza Michael Ntuyahaga mwaka 1959.
Mauaji yaliyotokea Rwanda mwaka 1960 yalliwafanya Watutsi wa Burundi wajihami.  Mwaka 1962 chama cha Watusi UPRONA kilichukua madaraka Burundi ilipopata Uhuru chini ya mwana mfalme Rwagasore, ambaye bahati mbaya aliuawa miezi michache baadaye.
Ingawa katika uchaguzi wa mwaka 1965 Wahutu walishinda, lakini madaraka yalichukuliwa na Watutsi.  Wahutu walipoasi wakipigania haki yao, viongozi 131 wa Kihutu na Wahutu wengine waliuawa na Kanali Micombero wa kabila la Kitutsi.
Baadaye Micombero alimpindua mfalme Ntare V.  Wahutu walinyanyaswa sana. Mwaka 1972 Wahutu walijaribu kujikomboa na kuwaua Watusi 1200.  Watusi walilipiza kisasi kwa kuwaua zaidi ya Wahutu 120,000 wakianza na wasomi.  Zaidi ya waalimu na Makatekista 2,300 Wahutu waliuawa.
Kanisa nchini Burundi lilisimama imara katika majaribu haya, kuna Watutsi wengi walioteseka au kuuawa wakiwalinda Wahutu, na Wahutu vilevile wakiwatetea Watutsi, kati yao wakiwemo Mapadre na Watawa. Hata hivyo hata wale waliokuwa wanaua walikuwa Wakristo.
Mwaka 1976 Jean Baptist Bagaza alimpindua Micombero. Bagaza alichukia Kanisa Katoliki. Aliwafukuza Wamisionari 300, akawafunga Mapadre 20, akapiga marufuku misa za kila siku na vyama vya kitume na kufunga Seminari zote.
Hata hivyo Kanisa liliendelea likitumia ukomavu wa Waamini wake katika kueneza Dini. Kwa wastani Padri mmoja alliwahudumia waamini zaidi ya elfu kumi na tano. Huu ulikuwa wakati mgumu kwa Kanisa, lakini ulilikomaza na kuliimarisha.
Kumekuwepo na  Maaskofu shupavu kama Askofu Simon Ntamwana wa Bujumbura, Mhutu, ambaye alipoteza karibu ndugu zake wote kwa kuuawa na Watutsi lakini bado anapigania amani kwa upendo na utulivu bila kuwa na kisasi.
Mwaka 1987 Pierre Buyoya, naye Mtutsi, alimpindua Bagaza.  Buyoya alikuwa mtu mstaarabu; alifanya amani na Kanisa na kushirikiana nalo, akawaingiza Wahutu katika Serekali yake na kutayarisha uchaguzi mwaka 1993.
Kutokana na uchaguzi huo Mhutu, Melchior Ndadaye, akiongoza chama cha FRODEBU, alichaguliwa kuwa Rais, ila miezi michache baadaye aliuawa na Jeshi la Watutsi lililoasi.  Rais Mhutu aliyemrithi aliuawa katika ndege iliyotunguliwa Rwanda pamoja na Raisi wa Rwanda Habyarimana.
Katika vita vya wenyewe kwa wenyewe, maelfu ya Watutsi na malaki ya Wahutu waliuawa. Mwaka 1996, Buyoya kwa mara nyingine tena alishika madaraka ya serikali na kidogo kuleta hali ya utawala, ingawa mapigano yaliendelea kwa sababu vikundi kadhaa vya Wahutu viliingia vita vya msituni.
Mazungumzo ya maelewano yalisimamiwa kwanza na Mwalimu Julius Nyerere, Raisi mstaafu wa Tanzania, na baada ya kifo chake yakasimamiwa na Mzee Nelson Mandela, Rais mstaafu wa Afrika ya Kusini, ambayo mwaka 2000 yalianza kuzaa matunda, na mwaka 2003 vikundi vikuu vilitia sahihi ya kusitisha mapigano.
Katika uchaguzi wa mwaka 2005 alishinda na kiongozi  waasi Pierre Nkurunziza wa chama cha CNDD-FDD. Ila chama cha Paripehutu, bado kiko msituni kikipigana.
Katika vita hivi Kanisa lilihusika kama mtume wa amani na uelewano, na limejaribu kufanya juhudi nyingi kupatanisha raia. Mwaka 2010 kati ya wakazi milioni nane, asilimia 65 walikuwa Wakatoliki, Waislamu asilimia 10 na Waprotestanti asilimia 5. Asilimia 20 zilizobaki za watu wa dini za asili, wengi wao wakiwa wakereketwa Wakatoliki ambao bado hawajabatizwa.
Uinjilishaji Kongo Brazaville:
Akishindana na Stanley, Sarvagnon de Brazza, aliweza kusimika bendera ya Ufaransa Kaskazini, mwa Mto Kongo na kushika sehemu yote ya Kaskazini na hivyo kuunda koloni za Kifaransa karibu na Ekweta. Koloni hizo zilikuwa Kongo-Brazaville, Gabon, Ubangi Shari (ambayo sasa ni Jamuhuri ya Afrika ya Kati) na Chad. De Brazza alipofanywa mtawala baada ya mkutano wa Berlin, aliwaalika Shirika la Roho Mtakatifu kuunda Vikariati.
Kufikia mwaka 1883 Wamisionari wa Shirika la Roho Mtakatifu walikuwa na misioni imara kwenye mwambao na katika mji wa Brazaville. Augourd alipewa Uaskofu mwaka 1894, na alifanya kazi kubwa ya uinjilishaji hadi alipokufa mwaka 1921.
Wakazi wengi wa Kongo-Braza ni wa kabila la ‘Bakongo’, watu wa dini waliomwita Mungu ‘Nzambi’. Hata leo nyimbo zao nyingi hata za kiraia humtukuza huyo Mungu wao. Kabila hili liko vile vile Kongo Kinshasa. Kutoka n’gambo ya mto kule Kongo-Kinshasa walipokea Wamisionari Waprotestanti kutoka Sweden mwaka 1909.
Kanisa hilo liliendelea vizuri sana. Tangu mwaka 1961 linaongozwa na Waafrika na Waamini wao leo wana asilimia 10 ya wakazi wote. Vile vile, kutoka Kongo Kinshasa walipokea dini ya Wakristo Waafrika ya Kibanguisti.
Kule Kongo Braza vile kulizaliwa dini nyingine za Kikristo za Kiafrika kama dini ya ‘Mungu wa Mshumaa’, na nyingine ya kisiasa iliyotaka kumkomboa Mwafrika kutoka katika ukoloni. Dini hiyo ilianzishwa na Andre Matswa. Matswa alifia gerezani chini ya Wafaransa, lakini Waamini wake wanamwona kama Messiha na wanangojea ujio wake.
Vile vile palikuwepo dini ya ‘kujipiga na Msalaba’ iliyoanzishwa na mkatekista Mkatoliki, Victor Malanda’ ambayo Waamini wake walipakwa mafuta kwa ajili ya kuacha ushirikina. Pia palikuwepo na dhehebu la ‘Jeshi la Wokovu,’ ambao alama yao ni bendera. Dhehebu hili la Wokovu ambalo ni kama maaskari liko katika nchi nyingi hata hapa Tanzania.
Licha ya madehebu mengi, Wakatoliki waliongezeka sana ingawa hawakufadhiliwa sana na serikali kama wenzao wa Kongo-Kinshasa katika kufadhili shule. Mwaka 1960 Kanisa lilimpata Askofu wake wa kwanza Mwafrika, Theophile Mbemba ambaye mwaka 1964 aliteuliwa kuwa Askofu Mkuu wa Brazaville.
Wakati huo Wakatoliki kwa uelekeo au mashabiki walikuwa asilimia 52 ya wakazi wote, wakifuatiwa na Waprotestanti asilimia 27, Makanisa ya kiafrika asilimia 9. Ingawa asilimia ni kubwa, kati yao kuna wengi waliokuwa washabiki tu wa Ukristo bila kujiunga rasmi kwa kubatizwa. Katika Sensa walijiandikisha katika madhehebu hayo. Mwaka 1973 Kongo-Brazaville ilipata Kardinali wake wa kwanza Emile Biayenda.

Rate this item
(0 votes)

Leave a comment

Make sure you enter all the required information, indicated by an asterisk (*). HTML code is not allowed.