DAR ES SALAAM
Na Mathayo Kijazi
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi amesema kuwa Wakristo wanapoadhimisha Misa Takatifu ya Jubilei, wanatakiwa kumtambua Mungu kama Baba wa Huruma, wa Hisani, na pia wa Upendo katika maisha yao.
Askofu Mkuu aliyasema hayo hivi karibuni wakati akihubiri katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya Parokia ya Bikira Maria Consolata, Kigamboni, iliyokwenda sanjari na utoaji wa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, na Sakramenti ya Ndoa Takatifu.
“Leo ni siku ya shangwe na shukrani kwa Mungu kutokana na mambo makuu ambayo ametutendea, kutokana na safari ambayo ametujalia kuifanya kama Wanaparokia wa Parokia hii ya Kigamboni:
“Na tunapofanya Adhimisho hili la Shukrani na Masifu kwa Mungu, tunaangazwa na kuongozwa na Neno la Mungu. Somo letu la Kwanza ambalo limetoka katika Kitabu cha Nabii Zefania, limetufundisha kwamba uhamishoni ni mahali pa mahangaiko, ni mahali pa kunyanyasika. Lakini Mungu ni mwaminifu, hata kama wamepelekwa uhamishoni kutokana na dhambi zao, dhambi haina kauli ya mwisho. Mungu anawaahidia mwanzo mpya …. Hata sisi tunaoadhimisha Miaka 50 ya Parokia hii, tunamtambua Mungu kama Baba wa Huruma, Baba wa Hisani, Baba wa Upendo.”
Katika homilia yake, Askofu Mkuu Ruwa’ichi alisema kuwa Mungu ni mwenye huruma katika maisha ya wanadamu, kwani licha ya mapungufu mengi waliyo nayo wanadamu hao, lakini yeye hawatupi, na anawapa tena fursa ya kuanza upya.
Aidha, aliwasisitiza Waamini kuitumia vyema kila fursa waliyopewa na Mungu, ikiwemo kujikusanya na kuamua kuanza upya, wakitambua kuwa kwa kufanya hivyo, ndiko kuudhihirisha ukuu wa Mungu katika maisha yao.
Wakati huo huo, Askofu Mkuu alisema kuwa katika Misa hiyo Mama Maria wanamwadhimisha kama Consolata, Mama mwenye Huruma, Mama Msaidizi, na pia kama Kimbilio na Mwombezi wao, huku akiwapongeza Wanakigamboni kwa kuzawadiwa Bikira Maria Consolata, kama Mwombezi na Msimamizi wao.
Pia, aliwaalika Wanaparokia hao kwa kuwa tayari, kwani wanaye Msimamizi mwenye uzito. Hivyo watumie nafasi hiyo kumuiga pamoja na kumpa nafasi ili waweze kuyatimiza mapenzi ya Mungu katika maisha yao, akiwapongeza kwa miaka 50 tangu kuwa Parokia mwaka 1973.
Pia, alisema kuwa wao ni wakongwe kwa sababu walipotangazwa kuwa Parokia, Jimbo lilikuwa bado halijafikisha hata Parokia 10, hivyo akawasisitiza kuutambua uzito walio nao, kwani hadi sasa zimefika 150, na Parokia Teule 24.
Kufuatia kauli hiyo, Askofu Mkuu aliwaasa kusimama kadri ya kimo chao, huku akiwataka kuonyesha nguvu yao, uwezo wao, uimara wao, pamoja na utayari wao wa kuwa mhimili wa Kanisa katika Jimbo hilo.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi aliwaasa Waimarishwa wa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara kumpokea Roho Mtakatifu ili awakamilishe katika Neema ya Ubatizo, na kuwapa utayari wa kwenda kumshuhudia Kristo.
Aliwasisitiza pia kuhakikisha kwamba Roho Mtakatifu wanayempokea, hawamhuzunishi, bali wanajipanga kutenda kazi pamoja naye katika maisha yao, akisema kuwa licha ya kwamba ni wadogo kiumri, kiimani ni wakubwa, hivyo wanahitaji kuendelea kuwekewa misingi imara.
Wakati huo huo pia Askofu Mkuu aliwapongeza wanandoa kwa kuchukua uamuzi huo wa kuachana na uchumba sugu, akisema kuwa kwa kufanya hivyo, wamelipokea jukumu la kuunda Kanisa la Nyumbani, pamoja na kuwa washiriki wa kazi ya uumbaji wa Mungu kitakatifu katika maisha yao.
Aliwakumbusha kuwa wito wao huo kama wanandoa, una mihimili yake ikiwemo upendo, uaminifu, na umoja, pamoja na kufahamu kwamba ndoa ya Kikristo ni ya mke mmoja na mume mmoja, na si vinginevyo. Hivyo akawasisitiza kuizingatia mihimili hiyo.
Parokia ya Bikira Maria Consolata, Kigamboni, ilitangazwa rasmi mwaka 1973, na kabla ya hapo ilianza kama Kigango cha Parokia ya Mtakatifu Yosefu, jimboni humo.