MWANZA
Na Paul Mabuga
Tunapaswa tujiulize tumekosea wapii, kama tunaona mkoloni aliweza hata mwalimu wenye ‘denge’ ni wetu. Ungana na Mwandishi Wetu, PAUL MABUGA, katika makala haya.
Uamuzi wa serikali wa kuwafanyisha mtihani walimu waliohitimu mafunzo ya taaluma hiyo kabla ya ajira kama ulivyotangazwa na Profesa wa Uchumi na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Fautine Mkenda ni jambo linalofikirisha na hata kufukarisha.
Inafikirisha na kufukarisha hisia kwa sababu, Walimu wanaofanyishwa mtihani ni wale ambao walipewa mafunzo na kufaulu na kisha kupata hadhi hiyo adhimu.
Ni lazima akili zifubae kwa sabau ukiwakuta walimu katika shule zetu katika nyakati hizi unakoma ubishi.
Unakuta mwalimu katika shule naye kanyoa nywele pembeni ya kichwa na kuziacha zikichanua kwa juu, hata zamani mnyoo wa aina hiyo ulikuwepo na ulikuwa maarufu kwa jina la denge.
Yaani kichwa kinakuwa ndege anayejulikana kama shole kibwenzi, ila walimu walikuwa hawawezi kunyoa hivi kwa ajili ya staha na haiba.
Profesa Mkenda amekakaririwa akisema Utaratibu huo, unalenga kurudisha hadhi ya taaluma ya ualimu, isitazamwe kuwa chaguo la mwisho baada ya kukosa nyingine na pengine katika mtazamo huo inategenewa kujibu baadhi ya malalamiko ambayo yamekuwa yakitolewa.
Yaani kile Waziri huyu alichokuwa akikiona kwa walimu wake wakati akiwa mtoto wa shule katika miaka ya sitini kule Rombo, sasa hakipo na kwamba hadhi ya taaluma hiyo imeshuka.
Kwamba mwalimu wa wakati huo alikuwa na hadhi ikilinganishwa na vijana wa kisasa.
Kwamba walimu wa kizazi cha elimu mkoloni na mchanganyiko kidogo wa Tanganyika huru walikuwa bora na wenye hadhi na wakifanya kazi yao barabara.
Wengi wao wakiwa wamevuka ile hali ya kuvaa kamptura safi na sasa wanavaa suruali lakini wamechana ‘way’ kwenye nywele kama wazungu. ‘Way’ ni kule kuchana nywele na kuachia ki njia upande wa kushoto.
Kwamba kutokea hapo, tukaja na kizazi cha walimu katika miaka ya 1980 na mwanzono mwa 1990, hapa kulikuwa na walimu kutoka vyuoni lakini pia na wale wa Azimio la Musoma ambao walikuwa wahitimu wa kidato cha sita na kulazimika kufanya kazi miaka miwili ikiwa ni pamoja na kufundisha kabla kwenda Chuo Kikuu.
Lakini pia kulikuwa na walimu ambao baada ya kuhitimu elimu ya msingi walisajiliwa kuwa walimu, huku wakiendelea kupata mafunzo nje ya vyuo kwa miaka mitatu, walijulikana kama UPE, kwa sababu walikuwa chini ya mpango wa Elimu kwa wote, [Universal Primary Education.
Hawa na wengine wote walikuwa na hadhi kuliko hali ilivyo sasa kama ilivyo dhania ya Profesa Mkenda kupitia utaratibu wa mtihani kabla ya ajira ya ualimu Je ni kweli hadhi ya Ualimu imeshuka?
Lakini kuna mtazamo mwingine! Inatokea tu, unapita katika mitaa ya mji Kahama, Mkoani Shinyanga, sehemu ambayo awali ilikuwa ikijulikana kama Uhindini, unaingia katika familia moja ya watanzania wenye asili ya India na unakaribishwa kwenye chai ya maziwa kwenye kikombe cha udongo.
Kisha anaitwa Bibi wa familia na unatambulishwa kwamba huyu ni mtoto wa mwalimu wetu. Unapata heshima hii kwa sababu ya baba yako na unamkumbuka alikuwa akipiga ‘way’ wakati huo.
Je kuna familia ngapi leo, zinawahusudu walimu kiasi cha kuwapa heshima inayodumu? Utawapaje heshima wakati visanga vya walimu vinatikisa taarifa kwenye vyombo vya habari!
Pale Mwalimu kazichapa ngumi na mwanafunzi, kule mwalimu kampa ujauzito mwanafunzi na walimu wamegoma kwa kucheleweshewa posho, huku wakiimba, ‘’ tunataka haki zetu.’’
Unaongea na mwalimu mmoja katika Shule ya Sekondari ya binafsi iliyopo katika Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga na anakuambia, “hawa walimu vijana waliomaliza Chuo Kikuu kwa siku hizi, tunawalipa mshahara wa Shilingi 200,000/-, kwa sababu uwezo wao mdogo na hawana ufanisi, ila wenye Diploma za zamani tunawalipa hadi Shilingi 800,000/-.”
Lakini waulize pia wanafunzi wa Sekondari waliopo ilikizo wakati huu kwamba, Walimu wanawafundisha masomo kwa lugha ipi, watakuambia masomo karibu yote yanafunddishwa kwa Kiswahili, iwe ni Biilojia, Basic Mathematics ama History, yote hayafundiswi kwa Kiingereza kama inavyitakiwa.
Mkuu mmoja wa Shule ya Sekondari anasema tunaletewa vijana ambao hawawezi hata kuongea Kiingereza katika mikuanyiko ya wanafunzi asubuhi sembuse kuandika barua ya kuomba ruhusa kwa Kiingereza.
Je mtihani ni suluhisho
Ni wazi kuwa kuna tatizo katika kuwatayarisha walimu na yote yanayolalamikiwa mchanganyiko wa mambo ambayo kwa bahati mbaya, jawabu lake siyo walimu kuwafanyisha mtihani kabla ya ajira.
Hii ni dawa isiyo na uwezo wa kutibu hata kama inaleta ahueni, [placebo]. Ni kwa sababu hailengi matatizo yaliyopo katika kuwatayarisha walimu.
Profesa Mkenda ajiulize, ni kwa nini kila Mwalimu anakuwa na jitihada na kusoma ili aweze kubadili kazi? Ajiulize ni kwa nini vyuo vyetu vinashindwa kutayarisha walimu wenye ubora na hata wanafaulu bila ya kuwa na viwango vinavyotakiwa? na kwa namna gani uwezo wa akili ya darasani unalingana na uwezo wa kufanya kazi yenyewe?
HIi ni kwa sababu hata wahuni wanaweza kufaulu mtihani huo wa ajira!Na wamejipangaje kutibu gonjwa lenyewe badala ya kuhangaika na dalili?
Wenzetu mwalimu akifuzu na kusajiliwa kuwa mwalimu, [staatsexament kwa ujeumani] kunakuwa hakuna shaka juu ya ubora wake.
Uaalimu ni taaluma nyeti, na ndiyo maana kunahitajika mfumo bora wa kuwatayarisha walimu, ikiwa tangu wakati wa kuchagua wanaingia chuoni!
Haiwezekani ukawa na mfumo wa kizembe na utegemee kupata walimu bora. Tujenge mazingira ya vijana waipende kazi na kuwa chaguo la kwanza.